Majadiliano ya makinikia yamefikia hatua nzuri

Dodoma. Waziri wa Sheria na katiba, Palamagamba Kabudi amesema majadiliano kuhusu mchanga wenye madini (makanikia) yamefikia hatua nzuri na Taifa litataarifiwa hivi karibuni.

Amesema hayo leo Ijumaa Novemba 24,2017 alipozungumza katika mkutano na wanasheria wa Serikali mjini Dodoma.

Acacia, kampuni tanzu ya Barrick na inayomiliki migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi, imezuiwa tangu Machi 2017 kusafirisha makinikia kwenda kuyayeyusha nje ya nchi kwa ajili ya kupata mabaki ya dhahabu, shaba, fedha na madini mengine yaliyoshindikana kuchenjuliwa migodini.

Baada ya majadiliano baina ya Serikali na Barrick, kampuni hiyo ya Canada imekubali kulipa dola 300 milioni “kuonyesha uaminifu” baada ya kutuhumiwa kukwepa kodi.

Kampuni ya Barrick imetenga dola 300 milioni za Marekani (zaidi ya Sh660 bilioni) kuilipa Serikali, lakini imeweka sharti; inataka iruhusiwe kusafirisha makinikia.

Wakati wa mkutano na vyombo vya habari uliofanyika Ikulu, Waziri Kabudi ambaye alikuwa mwenyekiti wa wawakilishi wa Serikali katika majadiliano alisema Barrick wamekubali kutekeleza masharti yote ya sheria mpya ya madini.

Mgogoro kati ya kampuni ya Acacia, mchimbaji na msafirishaji mkubwa wa dhahabu ya Tanzania, na Serikali ulishika kasi Machi baada ya kampuni hiyo kuzuiwa kusafirisha mchanga wa madini.

Baadaye Rais John Magufuli aliunda kamati mbili kuchunguza kiwango cha madini kilichokuwa katika makontena 270 yaliyokuwa Bandari ya Dar es Salaam, athari za kuusafirisha kwenda nje, sheria na mikataba.

Kamati hizo zilisema zimebaini kiwango cha dhahabu ni mara kumi ya kile kilichotangazwa na Acacia, kukwepa kodi na kukiuka sheria, huku mikataba ikionekana kunufaisha wawekezaji.

Ripoti hizo zilisababisha mawaziri kuwajibishwa na baadaye Serikali na Barrick kukubaliana kuunda timu za majadiliano, ambayo yalijikita katika muundo na mfumo mpya wa uendeshaji wa kampuni tanzu za Barrick, kubadilisha uendeshaji wa biashara ya madini na kuwanufaisha zaidi wananchi wanaoizunguka migodi.

Mengine ni kubadilisha mikataba ya madini (MDA) ili iendane na sheria mpya kwa lengo la kuongeza ushiriki na mapato ya Serikali, pamoja na kuainisha fidia ya makosa ya Acacia.

Walikubaliana kwa baadhi ya mambo na mengine majadiliano yanaendelea.