Upandikizaji figo wafanyika Muhimbili


Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Hospitali ya BLK ya nchini India imefanya upasuaji wa kwanza wa kupandikiza figo kwa mafanikio.

Upasuaji huo wa kwanza wa kihistoria wa upandikizaji wa ogani za mwili kuwahi kufanyika Tanzania umefanyika Jumanne Novemba 21,2017.

Taarifa ya awali iliyotolewa na Hospitali ya BLK leo Ijumaa Novemba 24,2017  imesema upasuaji huo umefanyika kwa mwanamke mwenye umri wa miaka 30 aliyekuwa katika hatua ya tano ya ugonjwa.

Imeelezwa upasuaji umefanywa na timu ya madaktari wa upasuaji, madaktari bingwa wa figo, wataalamu wa dawa za usingizi na wauguzi ikiongozwa na mkuu wa kitengo cha figo na magonjwa ya mfumo wa mkojo kutoka BLK, Dk Harden Singh Bhatyal.

Taarifa ya BLK imesema mwanamke huyo ambaye alishaingia katika huduma ya kusafishwa damu kwa mwaka mmoja sasa, amepatiwa figo na mdogo wake wa kiume mwenye umri wa miaka 27 aliyeamua kuokoa maisha ya dada yake.

"Mtoaji figo na aliyepandikizwa wote afya zao zinaendelea vizuri," imesema taarifa hiyo.