https://monetag.com/?ref_id=TTIb Simba yafanya maamuzi magumu | Muungwana BLOG

Simba yafanya maamuzi magumu


SIMBA SC imesajili wachezaji watatu wapya wa kigeni, beki Mghana Asante Kwasi, kiungo mshambuliaji Mzambia Jonas Sakuwaha na mshambuliaji Antonio Dayo Domingues kutoka Msumbiji.

Wakati dirisha dogo la usajili linakaribia kufungwa jana, viongozi wa Simba walikuwa wanahaha kukamilisha usajili huo, hususan wa mchezaji Kwasi, ambaye bado ana mkataba na klabu yake ya sasa, Lipuli ya Iringa.

Lakini kwa Sakuwaha na Domingues hakukuwa na tatizo na habari zinasema wachezaji hao watachukua nafasi za beki Mzimbabwe, Method Mwanjali na washambuliaji, Mghana Nicholas Gyan na Mrundi Laudit Mavugo. 

Wapinzani wao, Yanga wamesajili wachezaji wawili tu wapya, beki Fiston 'Festo' Kayembe Kanku kutoka Balende FC ya kwao, DRC na mshambuliaji kinda, Yohanna Nkomola ambaye ni mchezaji huru, aliyekuwamo kwenye kikosi cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys.

Azam FC imeingiza mmoja tu mpya, mshambuliaji Bernard Arthur kutoa Liberty Professional ya Ghana, baada ya kumuacha Mghana mwenzake, Yahya Mohammed na Singida United imesajili saba wapya; Lubinda Mundia kwa mkopo kutoka Res Arrows ya Zambia, Daniel Lyanga kutoka Fanja ya Oman, Kambale Salita 'Papy Kambale' kutoka Etincelles ya Rwanda, Issa Makamba, Assad Juma, Ally Ng’azi na Mohamed Abdallah wote huru waliokuwa Sereneti Boys.

Singida imewaacha wawili, Atupele Green na Pastory Athanas waliovunjiwa mikataba wakati Mohamed Titi na Frank Zakaria wametolewa kwa mkopo Stand United na Mbeya City imewasajili George Mpole kutoka Maji Maji na Abubakar Shaaban huru, baada ya kuwaacha Emmanuel Kakuti na mkongwe Mrisho Ngassa anayehamia Ndanda FC.