https://monetag.com/?ref_id=TTIb Waziri Mahiga apata mwaliko China | Muungwana BLOG

Waziri Mahiga apata mwaliko China

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga atafanya ziara ya kikazi nchini Jamhuri ya Watu wa China kuanzia tarehe 17 hadi 21 Desemba 2017 kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mhe. Wang Yi.

Balozi Mahiga anayetarajiwa kuondoka nchini tarehe 17 na kurejea tarehe 21 Desemba atatumia ziara hiyo kukutana na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa makampuni makubwa ili kujadili kwa pamoja namna pande mbili zitakavyoweza kushirikiana katika miradi ya kipaumbele ambayo itarahisisha kwa haraka Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kutimiza agenda ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2020.

Waziri Mahiga na ujumbe wake utakaojumuisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango wa Serikali ya Zanzibar, Bw. Khamisi Omari, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Thomas Kashililah na Naibu Katibu Mkuu wa Biashara na Uwekezaji kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Joseph Buchweishaija wataiomba Serikali ya China kushirikiana na Tanzania kuendeleza miradi ya kipaumbele katika sekta ya miuondombinu ya reli, viwanja vya ndege, bandari, nishati ya umeme, maji na uwekezaji wa viwanda

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kati ambapo Serikali ya China imeonesha dhamira ya kusaidia awamu zilizosalia. Aidha, licha ya Serikali ya awamu ya tano kudhamiria kujenga kituo cha kuzalisha umeme wa Mega-Watts 2100 katika Mto Rufiji (2100 MW Stigler’s Gorge Hydoropower project) kwa kutumia fedha za ndani lakini Ujumbe huo utaiomba China isaidie mradi huo ili Serikali iweze kuokoa fedha na kujikita katika miradi mingine.

Miradi mingine itakayojadiliwa ni pamoja na ujenzi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro, Mradi wa ujenzi wa njia ya kusambaza umeme wa KV 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, ukarabati wa Reli ya TAZARA na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ambao upo katika hatua za mwisho za maandalizi ili uweze kuanza mapema mwakani.

Balozi Mahiga na ujumbe wake umepangiwa miadi ya kuonana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mhe. Wang Yi, Naibu Waziri wa Biashara, Mhe. Qian Keming na mmoja wa viongozi wa juu wa Chama Tawala cha China, State Councillor Yang Jiechi.

Waziri Mahiga pia atatembelea na kufanya mazungumzo na watendaji wakuu wa makampuni makubwa ya China yakiwemo Sinolight ambayo pamoja na mambo mengine inajihusisha na ununuzi wa mihogo mikavu, Kampuni ya Foton Motors
group inayotengeneza magari ya bei nafuu na kampuni ya China Merchant ambayo inawekeza katika mradi wa Bandari ya Bagamoyo.

Kampuni zote hizo zimeonesha dhamira ya kufanya uwekezaji mkubwa hapa nchini ambapo utakapokamilika utatoa ajira nyingi kwa Watanzania na kuongeza mapato ya Serikali.