Mwalimu akamatwa kwa kumkashifu Rais Magufuli


JESHI la Polisi Mkoa wa Kagera linamshikilia mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Nyakisasa iliyopo Tarafa ya Rulenge wilayani Ngara, Deogratias Simon (34) kwa tuhuma za kumkashfu Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kupitia mtandao wa Facebook.

Mwalimu huyo anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya mwaka 2016 – 2018 kupitia mitandao ya kijamii ambapo inadaiwa alikuwa akisambaza ujumbe ambao polisi wanaona ulikuwa na lengo la kumchafua Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Augustine Ollom amesema kuwa mwalimu huyo anashikiliwa kwa kosa la kuikashfu serikali na kumkashfu Rais Magufuli  kuwa ni Dikteta na anaminya demokrasia.

Kufuatia tukio hilo, akiielimisha Wananchi kupitia Mashindano ya mpira wa miguu ya Polisi Jamii Cup 2018 yanayoendelea wilayani Ngara yenye kauli mbiu ya ‘’Kataa uhalifu, fichua wahalifu’’, Mkuu wa Jeshi la Polisi wilayani humo, Abeid Maige ameonya baadhi ya watu wasiopenda amani ya nchi hii wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii wakivunja shieria kwa kuahamasisha chuki dhidi ya Serikali.