https://monetag.com/?ref_id=TTIb Mwanza yapata neema, bilioni 2.6 kuboresha Afya | Muungwana BLOG

Mwanza yapata neema, bilioni 2.6 kuboresha Afya


Serikali imepeleka sh. bilioni 2.6 katika Jiji la Mwanza kwa ajili ya kugharamia uboreshaji wa vituo vya afya ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Hayo yalibainika jana (Jumanne, Februari 20, 2018) wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokagua na kuweka jiwe la msingi la kituo cha afya cha Karume.

Waziri Mkuu alikagua ukarabati wa kituo hicho kilichopo kwenye kata ya Bugogwa wilayani Ilemela akiwa katika siku ya sita  ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.

Alisema uboreshaji huo ulihusisha ujenzi wa chumba cha upasuaji, maabara, chumba cha kujifungulia, jengo la mama na mtoto na wodi ya wanawake na wanaume.

Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na uboreshaji wa kituo hicho, ambapo Serikali inatarajia kupeleka sh. milioni 200 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha inasogeza huduma za afya karibu na wananchi. Uboreshaji wa kituo cha afya cha Karume umegharimu takriban sh. milioni 497 hadi hivi sasa.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa  mkakati wa Rais Dkt. John Magufuli ni kuimarisha sekta ya afya ili kuhakikisha  wananchi wanapata matibabu karibu na maeneo yao ya makazi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndungulile alisema Serikali imetoa sh. bilioni 2.6 kwa ajili ya uboreshaji wa vituo vya afya jijini Mwanza.

Alisema fedha hizo zinalenga kuboresha vituo hivyo ili kuviwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi wa jiji zikiwemo huduma za afya ya mama na mtoto, upasuaji na maabara.

Awali, Waziri Mkuu alifungua zahanati ya Bulale iliyopo katika kata ya Buhongwa wilayani Nyamagana na kisha alitoa vitambulisho vya matibabu kwa wazee 250. Jumla ya wazee 5,398 wilayani humo wamepatiwa vitambulisho vya matibabu.