Wachapwa viboko hadharani kwa kujihusisha na ngono

Watu watano wakiwemo wanaume wawili na wanawake watatu, wamechapwa bakora hadharani nchini Indonesia, kwa kosa la kujihusisha na ngono kabla ya ndoa.

Tukio hilo limetokea Ijumaa ya April 20, 2018, ambapo imeelezwa kuwa watu hao wamevunja sheria za dini ya Kiislam, ambazo haziruhusu mtu yeyote kufanya ngono hadharani au nje ya ndoa na kuadhibiwa viboko 11 hadi 22.

Polisi wa masuala dini wa Indonesia (Sharia Police) walikusudia kuwafungulia mashtaka maalum ya kufanya ngono ambayo ni kinyume na sheria zao, ambayo ingewapelekea kupata adhabu kubwa zaidi, lakini walikosa ushahidi wanaostahili kuwa nao kuweza kuwahukumu.

Watu hao walionekana kulia kwa uchungu kutokana na maumivu makali ya bakora walizokuwa wakichapwa, lakini adhabu hiyo iliendelea kwa kila mmoja mpaka kumaliza idadi ya bakora zake.

Hata hivyo baadhi ya watu wa Indonesia wamesema sheria hiyo ni ya uonevu, na inakiuka misingi ya haki za binadamu.