Haji Manara atoa shukrani kwa niaba ya Simba

Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa Mabingwa wa Ligi Kuu (VPL) Simba SC, Haji Manara amefunguka na kuishukuru Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na Bodi ya Ligi kwa kuweza kuendesha michuano vizuri mpaka kupatikana bingwa bila ya kuwepo figisu figisu zilizo zoeleka kuwepo.

Manara ametoa kauli hiyo leo Mei 16, 2018 wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na kusema endapo asingetoa shukrani hizo kwa niaba ya wanasimba basi angekuwa mnafiki.

"Nisipo ishukuru Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi kwa niaba ya wanasimba nitakuwa mnafiki, kwasababu tulikuwa na tatizo kubwa la uozo kwenye mpira haipendezi kuirudia rudia lakini ni lazima niiseme. Bingwa alikuwa anaamuliwa kwenye twitter, ratiba zilikuwa zinapangwa mtandaoni mtu mmoja ndio alikuwa anaamua kila jambo, tulidhurumiwa sana Simba SC", amesema Manara.

Pamoja na hayo, Manara ameendelea kwa kusema "katika vitu ambavyo havitaweza kunitoka moyoni mwangu hili ni moja wapo la dhuruma, ujuha na uchizi wangu nilikuwa naonekana leo nimelipa na ndio maana Haji Manara maarufu kuliko msemaji yoyote Tanzania kwasababu wanasimba wana niamini na wanajua nimewapigania wakati tulipokuwa kwenye vita".

Kwa upande mwingine, Haji Manara ametoa ahadi kwa Rais Magufuli pamoja na mashabiki wa soka watakaofanikiwa kuingia uwanjani mnamo Mei 19, 2018 kuwa kikosi chake cha Simba kitatoa burudani ya aina yake ambayo haijawahi kutolewa tokea ligi kuu ilivyoanza.