5/16/2018

Hizi ndio sababu za Dewji kupewa Simba

Klabu ya soka ya Simba kupitia kwa Mwanasheria wake Evodius Mtawala, leo imeweka wazi sababu za mshindi wa zabuni ya kuwekeza kwenye klabu hiyo Mohamed Dewji, kupewa asilimia 49 ya hisa tofauti na 51 kama alivyotaka yeye.

Mtawala ameyasema hayo ikiwa ni siku chache zimebaki kuelekea kwenye mkutano mkuu wa klabu hiyo Mei 20 ambapo wanachama wataamua iwapo wanapitisha katiba mpya yenye kuruhusu mfumo wa hisa au la.

''Kwanza wanachama wanatakiwa kufahamu kuwa tayari  Mohammed ‘Mo’ Dewji amekubali kununua asilimia 49 ya hisa za klabu ya Simba SC na sio 51 kama aliyoomba awali na hii ni kwasababu ya kanuni na maelekezo ya Serikali'', amesema.

Mwanasheria huyo ambaye amewahi kuwa katibu wa Simba ameongeza kuwa wao kama klabu walikuwa tayari kuuza asilimia 50 mpaka 51 kwa bilioni 20 alizotoa Mo Dewji lakini baadae serikali iliagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.

Kwa upande wa wanachama, Mtawala amesema watamiliki hisa ndani ya kampuni ya 'Simba Sports Club Company Limited' kupitia kwa kampuni ya wanachama itakayoitwa 'Simba Sports Club Holding Company Limited' chini ya baraza la wadhamini.