Wastara afunguka tena

 Msanii wa kike wa filamu Bongo Wastara Juma amefunguka juu ya picha aliyopost instagram na kuzua mjadala kwa baadhi ya watu, huku wakimtuhumu kupanga njama za kutapeli kwa kutumia ugonjwa wake, ambao ulikuwa unamsumbua muda mrefu na kusababisha kupelekwa India kwa matibabu.

Akizungumza na www.eatv.tv Wastara amesema kwamba kitendo cha watu kumfikiria vibaya  kinamtia uchungu na kinamvunja moyo, kwani ukizingatia hakuomba kupata matatizo aliyopata, na kwamba picha aliyopost ni ya muda mrefu akiwa nchini India.

“Kwa kweli inasikitisha na inavunja moyo sana kama Mtanzania, na kama mtu ambaye nina haki zote kama wengine, hii ni picha ambayo niliipiga wakati nipo India,  na nafikiri nilieleza pia nilikuwa na matatizo ya kichwa, kwa hiyo ni moja ya kipimo na matibabu pia, kwa hiyo hiyo picha ni ya zamani wakati nipo India”, amesema Wastara.

Wastara amesema kwa sasa anaendelea vizuri na matibabu na hakuna tatizo linalomsumbua, hivyo watu wasitilie maanani maneno ya watu wanaomsema mabaya ili aonekane mbaya kwa jamii.