Azam FC usipime, yamrudisha staa wao nyumbani


Klabu ya Azam FC imefanikiwa kumrejesha kiungo wake, Mudathir Yahya kwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili kutoka Singida United.

Mudathir, kiungo Mzanzibar hodari leo amesaini mkataba huo mbele ya Makamu Mwenyekiti, Abdulkarim Amin ‘Popat’ na Meneja Philipo Alando, Mudathir alikwenda Singida United msimu uliopita baada ya kumaliza mkataba wake Azam na baada ya kazi nzuri akiwa na timu hiyo ya Uwanja wa Namfua amerejeshwa nyumbani.

Mchezaji huyo aliibuliwa katika mfumo wa soka ya vijana ya klabu hiyo, maarufu kama Azam Akademi mwaka 2013, kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza, ingawa baadaye ushindani wa namba ulimuweka kando.

Mudathir anakuwa mchezaji wa pili kusaini Azam FC kutoka Singida United ndani ya wiki mbili, baada ya Mzimbabwe Tafadzwa Kutinyu na kwa ujumla ni mtu wa tatu kutoka Namfua kuhamia Chamazi, baada ya kocha Mholanzi pia, Hans van der Pluijm.