6/13/2018

Gavana wa Nairobi amzungumzia Miguna Miguna


Gavana wa Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi Mike Mbuvi Sonko amesema atachagua mgombea mwingine nafasi ya Naibu Gavana wa Nairobi baada ya bunge la kaunti ya Nairobi, Jumanne hii kukataa uteuzi wake wa Mwanasheria Miguna Miguna.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Sonko amesema atatoa jina jingine baada ya "ushauri wa kutosha."

"Nitawasilisha mteule mwingine aliyestahili kwenye bunge la kaunti ya Nairobi baada ya kushauriana kwa kuhakikisha kuwa Nairobi inapata Naibu  Gavana anayestahili kusaidia katika utoaji wa huduma," amesema Sonko.

Aidha ameeleza kwamba "Ninataka kukubali uamuzi wa bunge la kaunti ya Nairobi kukataa uteuzi wa Dk Miguna Miguna kama Naibu Gavana wa Nairobi kwa sababu ya uraia kama ilivyoelezwa kwenye  kifungu cha 78 cha Katiba."

Mbali na hayo Spika wa bunge Beatrice Elachi,  Jumanne hii  alielezea kwamba hakuwa na uwezo wa kujadili uteuzi wa Miguna kwa sababu afisa wa Serikali hawezi kushikilia uraia miwili.

Hata hivyo Serikali ya Kenya  imesisitiza mara kwa mara kwamba Miguna si raia wa Kenya, kwa hivyo, ataruhusiwa tu kuingia nchini humo kwa kutumia pasipoti yake ya halali ya Canada.

Katibu Mkuu wa Uhamiaji Gordon Kihalangwa alisema Miguna lazima aomba tena upya kurejesha uraia wake nchini Kenya.

Mei 17 mwaka huu Gavana Sonko alimpendekeza Mwanasheria Miguna kuwa Naibu Gavana wa Mji wa Nairobi.