Kesi ya Wema Sepetu na wenzake yahairishwa hadi Juni 19


MUIGIZAJI wa filamu nchini, Wema Sepetu, leo alifika mahakamani baada ya kudaiwa akitokea India alikokwenda kufanyiwa upasuaji kama ilivyoelezwa na mama yake katika mahakama hiyo wakati wa mwendelezo uliopita wa kesi hiyo.

Msanii huyo alifika na wafanyakazi wake wawili wanaokabiliwa na kesi ya kutumia dawa ya kulevya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  wataanza kujitetea Juni 19, mwaka huu.

Wema na wenzake walipaswa kuanza kujitetea leo Juni 13 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba,  na kwa upande wa mawakili ni Cosstantine Kakula wa Serikali na Wakili wa Utetezi, Albert Msando.

Hata hivyo,  ilishindikana washtakiwa hao kuanza kujitetea kwa sababu Hakimu Simba alikuwa na kazi nyingine na kesi imeahirishwa hadi Juni 19, mwaka huu ambapo washtakiwa wataanza kujitetea.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Hakimu Simba kupitia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi watano wa upande wa mashtaka waliokuwa wakiongozwa na Kakula na kutoa uamuzi uliowaona washtakiwa hao wana kesi ya kujibu na hivyo wanapaswa kujitetea.

Mbali na Wema washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ya kutumia dawa za kulevya ni Angelina Msigwa na Matrida Seleman Abbas.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa za kulevya.