Makonda aanza kutekeleza agizo la Rais Magufuli


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ameanza kufanyia kazi agizo la Rais Dr. John Magufuli la kufuatilia taratibu za ujenzi wa Barabara ya kutokea Makao Makuu ya BAKWATA hadi Biafra na tatizo la mfumo wa maji kwenye eneo la Kinondoni Shamba.

Mapema leo  Makonda amefanya ziara ya ukaguzi na kubaini nyumba nyingi kwenye eneo hilo zimejengwa kwenye hifadhi ya barabara na baadhi ya watu tayari wamelipwa fidia ambapo amewataka wananchi kushirikiana na TARURA kuhakikisha ujenzi wa barabara unaanza Mara moja.


Aidha Makonda ameagiza TANESCO, DAWASCO na TTCL kushirikiana kwa karibu na TARURA kuondoa miundombinu yao ili kasi ya ujenzi uanze.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA Kinondoni Bwana Leopold Runji amesema tayari wameanza utekelezaji wa maagizo waliyopatiwa na watahakikisha ujenzi unaenda kwa kasi na kukamilika kwa wakati.



Itakumbukwa siku ya Jana June 12 Rais Dr. John Magufuli alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Msikiti na maendeleo ya ujenzi wa Makao Makuu ya BAKWATA ambapo wakati wa kuondoka alipata wasaha wa kuzungumza na Wananchi ambao waliwasilisha kwake ombi la ujenzi wa Barabara.