Mama Samia awataka wanasheria kusaidia wanawake


Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka watendaji wa sekta ya sheria kutumia taaluma zao kusaidia upatikanaji wa haki za wanawake na watoto ambazo licha ya nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania kuweka sheria zinazolenga kusaidia makundi hayo , changamoto bado ni kubwa na malengo yaliyotarajiwa hayajafikiwa.

Akizungumza wakati anafungua Mkutano wa Kimataifa wa majaji wakuu wa nchi za Afrika unaofanyika Arusha Makamu wa Rais amesema kuna haja ya majaji kuongeza umakini wakati wa kutoa mamuzi hasa yanayowahusu wanawake na watoto ambao asilimia kubwa ya makosa wanayofanya yanachangiwa na sababu zilizoko nje ya uwezo wao.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mh Profesa Ibrahimu Juma pamoja na kukiri kuwepo changamoto nyingi katika sekta ya sheria amesema jitihada za kuzikabili zinaendelea zikiwemo za kuendelea kujenga misingi ya kurahisisha upatikanaji wa haki kwa makundi yote wakiwemo wanawake .

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Kenya Steven Maraga amesema upo uwezekano wa kupunguza changamoto za masuala ya upatikanaji wa haki katika nchi za Afrika kama majaji wakiweza kushirikiana na kufanya kazi pamoja.

Baadhi ya watendaji wa Sekta ya sheria nchini Tanzania wameelezea baadhi ya changamoto zinazochangia kuendelea kuwepo kwa malalamiko licha ya kuwepo kwa jitihada kubwa za kuboresha sekta hiyo