Serikali yatoa tamko Mtanzania anayechezea Denmark Kombe la Dunia

Mtanzania huyo mwenye uraia wa Denmark, ameweka historia katika fainali hizo nchini Russia, baada ya kufunga bao pekee dhidi ya Peru.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Nchini Yusuph Singo, amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuweka utaratibu maalumu wa kutambua wachezaji wote wenye asili ya Tanzania wanaocheza nje ya nchi.

Singo alisema shirikisho hilo ndilo lenye dhamana ya kujua idadi ya wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaocheza Ulaya ambao watawekewa utaratibu na Serikali ili kuitumikia timu ya Taifa.

Mchezaji huyo katika jezi amekuwa akitumia jina la Poulsen, lakini amebadili na kuweka jina la baba yake, Yurary anayetoka mkoani Tanga. Awali, Poulsen alinukuliwa akidai ameshindwa kuitumikia Taifa Stars kwa kuwa hakuwahi kuitwa licha ya mara kwa mara kurejea nchini kuitembelea familia yake mkoani Tanga.