6/13/2018

Serikali yawataka wabunge kutoa elimu kwa wasichana


Serikali imewataka wabunge na wananchi kwa ujumla kusaidia kutoa elimu kwa wasichana nchini kutojiingiza katika vitendo vya ngono wakiwa katika umri mdogo ili kusaidia kupunguza mimba za utotoni.

Hayo yamesemwa leo Juni 13, 2018 Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, Ummy Mwalimu na kutoa wito kwa wasichana kuacha tabia ya kujiingiza katika vitendo vya ngono kabla ya kufika miaka 18 na kuongeza kuwa asilimia 14 ya wasichana hujiingiza katika vitendo vya ngono wakiwa chini ya miaka 15.

“Wasichana wajizuie kuingia katika vitendo vya ngono mpaka pale watakapofikisha umri wa miaka 18, kwakweli hali sio nzuri asilimia 14 ya watoto wa kike wanaanza ngono kabla ya hawajafikisha umri wa miaka 15, na watoto wa kiume ni asilimia 9, naomba waheshimiwa wabunge mtusaidie katika kuelimisha wasichana hasa kujizuia kufanya mapenzi kabla hawajatimiza umri wa utu uzima” amesema Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy ameongeza kuwa, tafiti zinaonesha zaidi ya asilimia 27 ya watoto wa kike nchini hupata ujauzito kabla ya kutimiza umri wa miaka 18 na hivyo kufanya idadi ya mimba za utotoni kuongezeka.

Waziri wa Afya alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Mpanda Mjini (CCM), Sebastian Kapufi aliyetaka kujua ni kwa namna gani Serikali itasaidia kupunguza mimba za utotoni hasa katika mkoa wa Katavi ambapo mimba za utotoni zimefikia asilimia 47.