6/13/2018

UDSM yatangaza ratiba ya kuaga miili ya watumishi, wanafunzi wake


Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), imetoa taarifa ya kukatisha ratiba ya masomo kwa muda wa masaa matatu kesho Juni 14, 2018 ili kutenga muda wa kuaga miili ya waliokuwa wanafunzi na watumishi wa chuo hicho.

Taarifa hiyo imetolewa leo Juni 13, 2018 na Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma Profesa Bonaventure Rutinwa na kuongeza kuwa masomo yatasitishwa kuanzia Saa 4:00 asubuhi mpaka 7:00 Mchana.

Taratibu za kuaga miili ya marehemu zitafanyika katika ukumbi wa Nkrumah uliopo chuoni hapo siku ya kesho Juni 14, 2018 kuanzia Saa 4:00 Asubuhi.

Katika ratiba ya kutoa heshima za mwisho kwa marehemu hao inaonesha, waombolezaji wataanza kuingia katika ukumbi wa Nkrumah kuanzia saa 3:00 asubuhi, na ikifika 3:45 miili ya marehemu hao itaingia ukumbini, ambapo shughuli ya kuaga itaanza rasmi saa 5:40 asubuhi mpaka 6:50 Mchana.Juni 11, 2018 katika eneo la Riverside-Ubungo wanafunzi wawili na watumishi wawili wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), walifariki Dunia baada ya gari la wagonjwa walilokuwa wamepanda kugoganga na lori la mizigo walipokuwa wanaenda katika Hospitali ya Chuo hicho kwa matibabu.

Waliofariki kutokana na ajali hiyo ni wanafunzi Erasto Sango Steven na Mary Godian Soko na watumishi wawili James Rutayuge ambaye alikuwa ni dereva pamoja na muuguzi msaidizi daraja la pili Jonathan Lung’ando.