Usajili mpya wa yanga noma


Usajili Yanga ni noma kwani kila kitu kuhusu nani anaachwa, anatolewa kwa mkopo na maingizo mapya kikosini humo yatajulikana leo baada ya uongozi wa timu hiyo utakapokutana na Kocha Mkuu raia wa DR Congo, Mwinyi Zahera.

Katika usajili wa msimu huu, majina ya wachezaji wanaotajwa kuwa watasaini mkataba mpya wa kuichezea timu hiyo ni Muivory Coast, Pascal Wawa, Juma Nyosso, Haruna Moshi ‘Boban’ na Mrisho Ngassa, Marcelin Degnon Koupko kutoka Benin, kipa wa zamani wa TP Mazembe, Vumi Ley Matampi na wengi kibao.

Pia Yanga itawasaini baadhi nyota waliomo kikosini humo ambao wamemaliza mikataba yao kama Kelvin Yondani, Juma Abdul, Hassan Kessy, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na wengineo.

Yanga hivi karibuni ilitangaza kamati yake mpya ya usajili iliyokuwa inaongozwa na Abbas Tarimba, Abdallah Bin Kleb na Hussein Ndama.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumamosi imezipata, katika kikao hicho kocha huyo anatarajia kukabidhi orodha ya wachezaji wapya anaotaka wasajiliwe, kuachwa na kutolewa kwa mkopo.

Mtoa taarifa huyo alisema, kocha jana alitarajiwa kuwasili nchini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gor Mahia utakaopigwa Julai 17, mwaka huu.

“Kocha wetu alikuwepo mapumzikoni nyumbani kwake Ufaransa alipokwenda kwa ajili ya mapumziko ya wiki mbili na leo (jana) usiku alitarajiwa kurejea nchini.

“Mara baada ya kurejea haraka kesho (leo) tutafanya naye kikao kujadili masuala mbalimbali ya usajili ukiwemo mahitaji ya wachezaji wake wapya atakayayotoa kwa uongozi.

“Baada ya hapo haraka tutaanza usajili huo wa wachezaji wapya kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chetu ili kuhakikisha tunarejesha heshima yetu ya timu iliyopotea kwa muda mrefu,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa kuzungumzia hilo, alisema: “Tumepanga kutangaza usajili wetu mara baada ya kufanya kikao na kocha wetu.

“Kikao hicho tumepanga kukifanya baada ya kocha kurejea nchini alipokwenda nyumbani kwake nchini Ufaransa kwa ajili ya mapumziko.”