Wasiodai risiti sasa kukiona cha moto


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeonesha ukali wake kwa wasiodai risiti kwa kumtoza faini dereva mmoja wa bodaboda baada ya kujaziwa mafuta kwenye pikipiki yake na kuacha kuchukua risiti ya kielekitroniki ya EFD.

Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere Jumamosi iliyopita akiwa katika doria, alimkamata ‘laivu’ dereva huyo aitwaye Issa Athumani na kumtoza faini papo kwa papo ya shilingi 30,000 baada ya kununua mafuta ya bodaboda hiyo bila kudai wala kuchukua risiti ya kielekitroniki ya EFD.

Kichere alisema kuwa, wananchi ambao hawadai risiti wanatakiwa kutozwa faini ya shilingi 30,000 hadi 1,500,000 au kuhukumiwa kifungo kisichozidi miezi sita kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015.

“Kuna watu ambao hawadai risiti na kuna mwingine nimemkamata leo (Jumamosi) ambaye nimemtoza faini ya shilingi 30,000 ili iwe fundisho kwa watu wote wanaonunua bidhaa na huduma mbalimbali bila kudai wala kuchukua risiti,” aliongeza Kichere.

 Aidha, Kamishna Mkuu Kichere ametoa wito kwa wafanyabiashara kuendelea kutoa risiti kila wanapofanya mauzo na wananchi kuhakikisha wanadai risiti kila wanapofanya manunuzi mbalimbali.

Wiki iliyopita Kichera pia alikamata na kutaifisha boksi 41 za mvinyo na pombe kali zilizokutwa katika duka la jumla jijini Dodoma la Anthony George zikiwa hazina Stempu za Kodi.

Akizungumza mara baada ya kutaifisha boksi hizo, Kichere amesema kuwa, ni wajibu wa muuzaji kuhakikisha kwamba, vinjwaji vinavyostahili kuwekewa Stempu za Kodi vinakuwa na stempu hizo ili kuisaidia Mamlaka kutoza kodi stahiki