Bandari bubu 200 zatumika kufanyia biashara ya unga


Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA ) imebaini uwepo wa bandari bubu zaidi ya 200 hapa nchini ambazo baadhi yake zinadaiwa kutumika katika biashara za magendo, usafirishaji wa dawa za kulevya na matishio ya kiusalama, hatua ambayo imeilazimu mamlaka hiyo kutoa muda wa hadi juni mwaka ujao kuanza kuzifungia bandari hizo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ngazi za wilaya na mikoa katika mkakati wa kudhibiti mapato ya serikali.

Hayo yameelezwa na mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya usimamizi wa bandari nchini Mhandisi Deusdedith Kakoko, wakati wa ziara ya waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe mkoani Mwanza iliyoanza julai 11, kwa waziri huyo kutembelea katika karakana ya kampuni ya Songoro Marine inayojenga kivuko kipya cha Mv. Mwanza kitakachotoa huduma ya usafiri kati ya Kigongo – Busisi mkoani humo.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa kivuko hicho, ambacho kipo hatua za mwisho kuanza kutoa huduma ya usafiri wa abiria na mizigo wakati wowote kuanzia wiki ijayo, waziri huyo wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kivuko hicho kitasaidia sana kupunguza msongamano wa abiria na magari uliopo kati ya Kigongo - Busisi kutokana na vivuko vitatu vilivyopo kwa sasa kuonekana kuzidiwa uwezo wake

Mkurugenzi wa kampuni ya Songoro Marine, Majoro Songoro amemhakikishia waziri huyo wa ujenzi kwamba kampuni hiyo ya kizalendo kwa sasa ina uwezo mkubwa wa kujenga meli kubwa ya zaidi ya tani 5000 na abiria zaidi ya 2000 mahali popote katika bahari na maziwa hapa nchini, hivyo ameiomba serikali iendelee kuiamini na kuipa kandarasi kampuni hiyo.