https://monetag.com/?ref_id=TTIb Esther Matiko awaza kuweka rekodi ya pekee yake | Muungwana BLOG

Esther Matiko awaza kuweka rekodi ya pekee yake


Baada ya kuandika historia ya kwanza kuwa Mbunge wa kwanza mwanamke kutoka kwenye jamii ya Wakurya, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko (CHADEMA) amesema kwamba anaamini atakuja kuipindua historia hiyo tena kwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke kutokea Tarime.

Esther Matiko ameweka wazi nia yake hiyo mapema jana alipokuwa katika kipindi cha KIKAANGONI kina chorushwa kupitia ukurasa wa Facebook EATV kila Jumatano ambapo ameeleza kwamba ameshapata maono ya kuwa siku moja atakuwa Rais wa Tanzania.

Matiko ameeleza kwamba "Sina ndoto tu za kuwa mgombea wa urais, bali naamini ipo siku nitakuwa Rais wa kwanza wa Tanzania mwanamke kutokea Tarime na kufanikiwa kuibadilisha historia upya. Kama nilivyoamini kwenye ndoto yangu ya darasa la nne kwamba ipo siku nitakuwa mbunge basi ndivyo ambavyo nitakavyoishi kwenye maono ya kuwa rais maana sitegemei kuishia kwenye nafasi ya ubunge. Nina ndoto kubwa ya kuitimiza".

Akizungumzia kuhusu ushindi wake wa Tarime Mjini ulitokana na kubebwa na chama chake, Matiko ameeleza kwamba anaamini kwakuwa wananchi walimuhitaji ndiyo maana chama kilimuamini, hivyo hata kama chama kingekuwa na umaarufu kama wananchi wasingemtaka basi hangeweza kufanikiwa hivyo anaamini wananchi na chama wote walihusika katika kumpatia yeye nafasi ya kutimiza ndoto zake.

Esther Matiko ambaye 2015 aliandika historia ya kuwa Mbunge wa kwanza kutoka Tarime mwanamke tangu kuanza kwa siasa za Tanzania na kwa kupitia chama cha upinzani amesema kwamba heshima aliyopatiwa na wananchi wa jamii yake hawezi kuisahau na shukrani zake ataziweka kwenye kitabu chake ambacho kwa sasa bado anakiandika.

Harakati za Matiko  za kugombea ubunge zilianza mwaka 2008 katika mchakato wa kumpata mgombea wa kuziba nafasi ya aliyekuwa mbunge wa jimbo la Tarime, Marehemu Chacha Wangwe ambapo katika mchakato wa chama hakuweza kupita.

Hata hivyo 2010, Matiko alipata nafasi ya kuteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa mara kwanza kutoka  Mkoa wa Mara nafasi ambayo ilimpatia fursa ya kuweza kuchukua jimbo la Tarime Mjini mwaka 2015.

Katika uchaguzi Mkuu wa 2015, Esther Matiko alifanikiwa kubadilisha dhana ya kwamba mwanamke hawezi kuongoza wakurya kwa kushinda nafasi ya ubunge kwa kura 20,017 na kumshinda mpinzani wake Kembaki Michael Mwita wa CCM, aliyepata kura 14,025 ambapo pia alikuwa mgombea wa kwanza Tanzania matokeo yake ya ushindi kutangazwa.