7/11/2018

Sumu Inayoathiri Mafanikio Ya Wengi


Hivi Uliwahi kukaa chini na kujiuliza hivi ni kwanini baadhi ya mambo mengi hufeli zaidi kuliko kuwa katika ubora ambao mtu ametarajia? Kama hujawahi kujihoji ipo haja zaidi ya kuushirikisha ubongo wako muda huu katika kuyafakari hayo ili kujua kwa undani zaidi.

Watalamu wa saikolojia wanazidi kututabainisha ya kwamba uwezekano mkubwa wa jambo lolote ambalo unalitaka kulifanya au unalifanya matokeo yake yasiwe kama vile ambavyo ulitaraji awali. Hata hivyo watalaamu hao hao wanazidi kutukumbusha ya kwamba Mambo mengi huwa yanafeli zaidi kuliko kuwa bora hii ni kutokana kutokuwepo kwa hamasa ya kutosha aliyo nayo mtu katika kulitenda jambo fulani.

Hamasa hii imsukumayo mtu katika kulitenda jambo fulani ndiyo sumu ambayo inayaathiri mafanikio ya wengi wetu kwa kiwango kikubwa sana. Ukichunguza kwa amakini katika safari yeyote ya kuyasaka mafanikio mwanzoni huwa ni safari yenye utamu mwingi kuliko uchachu .

Utamu huo ambao nauzungumzia ni kwamba kila mtu wakati anaanza kulitenda jambo fulani huwa yupo katika hali ya kulipenda sana jambo hilo, hata hivyo ndipo tunapoona ya kwamba hamasa isukumayo mtu katika kulitenda jambo hilo huwa kubwa sana, lakini licha ya hamasa hiyo kuwa  kubwa huanza kupungua siku hadi siku hii hutegemea na kiwango cha changamoto ambazo zitajitokeza.

Hebu tujikite kidogo kwa kuona baadhi ya mifano itakayotusaidia kutafakari.
a) Hebu tujiulize ni mahusiano mangapi leo hii yamekufa? Huku mitazamo ya watu wengi hawakutegemea kama mahusiano hayo yatakufa?

b) Ni biashara ngapi ambazo zilianza vizuri lakini kadri siku zinavyozidi kusonga nazo zinalegalega?

c) Ni wanafunzi wangapi ambao leo wameacha kuendelea na masomo yako lakini mwanzoni wakati wanaanza masomo walikuwa wanafanya vizuri? Achilia mbali sababu za  kutokuwapo na fedha kwa masomo bali jikite zaidi katika kutafakari sababu zile za kawaida kabisa.

c) Jiulize tena kwanini mara nyingi vipaji vingi vya watu hufa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele?

Kwa hayo machache kati ya mengi  ambayo umeyatafakari au unatakiwa kuyatafakari utagundua sababu za kufeli kwake ni Kutokana na muhusika huyo kukosa hamasa ya kupenda jambo hilo.

Lakini vilevile zipo changamoto kubwa na nyingi ambazo hujitokeza katika jambo hilo. Na kutokea kwa changamoto hizo ndizo ambazo zikekuwa sumu kubwa sana ambazo zinawafanya watu wengi kukakata tamaa mapema.

Nini kifanyike ile kuongeza hamasa za kiutendaji ili kufanikiwa?

1. Lifanye jambo lolote kwa upendo na sio kwa hofu au kwa kujaribu.
Upendo wa jambo lolote ambalo unalifanya linakufanya wewe kuweza kuwa katika hali ya ushindi wa mafanikio yako. Kupenda kitu kunakufanya kujua mbinu ambazo zitakusaidia kukabiliana na changamoto ambazo zitajitokeza.

Kwa mfano kama unataka kukua kibiashara lazima ipende kwa dhati biashara yako lakini ukiweka chuki kati yako na biashara yako biashara nayo itaweka chuki nawe, na kufanya hivi ni kutengeneza mazingira ya kufa kwa biashara yenyewe.

2. Zifanye changamoto kama njia za kukifikisha kwenye lengo lako.
Kila jambo lolote lina changamoto zake hivyo huna budi kuziogopa changamoto hasa chamgamoto zitakazokufanya ushindwe kufika kwenye Ndoto zako kubwa. Jambo la msingi zifanye changamoto kama njia ya kufika kule utakako, Huna haja ya kuacha kufanya jambo lolote lenye kukuletea mafanikio ambalo unalitaka kulifanya kwa sababu  ambazo sio msingi katika kukamilisha Ndoto zako.

3. Fanya kitu ambacho unakiogopa.
Ili uweze kufanikiwa huna budi kutokugopa kufanya jambo lolote. Kuacha au kugopa kufanya jambo lako ni dalili tosha kwamba huna hamasa za kiutendaji pia kufanya hivi kunakufanya kwa asilimia kubwa kuweza kufa na ndoto zako.

Lakini nikukumbushe ya kwamba idadi kubwa ya watu ambao wamefanikiwa katika sayari ni kwamba walifanya vitu ambavyo walikuwa wanaviogopa na mambo hayo ndiyo yaliyosaidia kugeuza maisha yao kwa asilimia kubwa.

Na watu hao wenye mafanikio huwa hawasimamishi maskio yao kusikiliza nani kasema nini, hususani wale wakatishaji tamaa. Tabia hii ya watu walifanikiwa ukiitumia leo itakusaidia sana.

Hivyo nikutie moyo kwa kukwambia ya kwamba Ndoto zako zinakwenda kuwa kweli endapo utakwenda kuijenga misingi imara ya hamasa za kiutendaji kwa jambo lolote lile ambalo unalifanya au unataka kulifanya.