Ugomvi wasababisha kocha na wachezaji 13 kufungiwa maisha


Shirikisho la mchezo wa kikapu Dunia (FIBA) hii leo limetangaza kuwafungia maisha wachezaji 13 na kocha baada ya kuzuka kwa ugomvi katika mchezo wa kufuzu fainali za Dunia za mchezo huo kwa upande wa bara la Asia kati ya Ufilipino na Australia uliofanyika mwezi huu.

FIBA imewafungia wachezaji 10 wa Ufilipino kutocheza michezo 35 huku wachezaji watatu wa Australia wakifungiwa jumla ya michezo tisa.

Vyama vya mchezo wa kikapu vya nchi zote pia vimetozwa faini, Australia ikitozwa faini ya Pauni 76,681 sawa na fedha za kitanzania Shillingi millioni 227,238,774 huku timu ya taifa ya Ufilipino ikitozwa Pauni 191,703 ambazo ni sawa na Shillingi millioni 568,021,968 za kitanzania na kuamriwa mchezo ujao wa nyumbani kucheza bila ya mashabiki .

Pia kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ufilipino, Vicent ‘Chot’ Reyes amesimamishwa mchezo mmoja na kutozwa faini ya Pauni 7,668 ambazo ni sawa na Shillingi millioni 22,721,050 za kitanzania .

Shirikisho hilo pia limemuondoa mwamuzi wa mchezo huo katika ratiba zijazo za shirikisho na hatochezesha mchezo wowote kwa muda wa hadi mwaka mmoja.

Ugomvi huo uliibuka Julai,2 mwaka huu katika robo ya tatu ya mchezo ambao Australia ilishinda kwa alama 89-53 ambapo wachezaji zaidi ya tisa wa timu mwenyeji waliingia uwanjani na kuzua ugomvi ambao ulichukua dakika 30 kuamuliwa kabla ya kuendelea tena.