Ahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kulawiti


Mahakama ya Wilaya ya Lindi imemuhukumu, kifungo cha maisha mwanaume mmoja aitwaye Mussa Milanzi mwenye umri wa miaka 29, baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka mitano.

Hakimu wa mahakama hiyo Erasto Phili, alitoa hukumu hiyo Ijumaa ya Agosti 17, 2018, baada ya kuridhika na ushahidi wa kitaalamu wa idara ya afya na upande wa mashtaka. Ambapo kabla ya hukumu hiyo mshtakiwa huyo alitoroka baada ya kupewa dhamana na kwenda kujificha Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara, ambako alikamatwa na kurejeshwa mkoani Lindi.

Awali Mwanasheria wa Serikali, Yahaya Gumbo aliiambia mahakama hiyo kwamba Oktoba 11, mwaka jana mchana, mshtakiwa akiwa kwenye kazi yake ya kuchunga ng'ombe eneo la pori la Angaza, Manispaa ya Lindi, watoto walikuwa wakimfuata nyuma na mifugo yake ndipo alipomkamata mmoja wao na kumlawiti.

Mshtakiwa huyo alipotakiwa kujitetea, aliiomba mahakama imuonee huruma kwa kuwa ana mke na mtoto mchanga na kwamba akipewa adhabu hiyo watakosa huduma yake.

Alidai kuwa alifanya kitendo hicho kutokana na kupitiwa na upepo mbaya.

Baada ya utetezi huo, Mwanasheria wa Serikali Yahaya Gumbo, aliiomba mahakama kumpa mshtakiwa huyo adhabu kali ili iwe fundisho kwake na wengine wenye tabia kama hiyo, ikizingatiwa amefanya unyama huo kwa mtoto asiyeelewa kitu chochote.