Hii ndio sababu ya baadhi ya Channel kuondolewa kwenye Ving'amuzi


Serikali imetoa ufafanuzi juu ya mkanganyiko na sintofahamu iliyoibuka kwa watumiaji wa vinag’amuzi vya multchoice- DSTV, Zuku na Azam kuhusu kutakiwa kuondoa channel za televisheni zinazotazamwa bila malipo ikiwemo Channel ten, Itv, Clouds Tv, na EATV.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar salaam waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Mhandisi Isaac Kamwelwe amesema hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni kulinda sheria na taratibu ambazo mamlaka ya mawasilino Tanzania TCRA ndio watekelezaji na kutoa wito kwa kila mwenye leseni kuheshimu sheria huku akiwahimiza wananchi kutumia ving’amuzi sahihi ili kupata huduma za maudhui ya bila malipo yaani free to air – FTA.

Mhandisi Kamwelwe amesema jana vyombo vya habari vilivyotajwa hapo juu vilitoa tamko la maoni yao kuhusu kadhia hiyo amebainisha kuwa licha ya kwamba sheria ilivunjwa haiwezi kuendelea kuvunja ingawa amesema ipo nafasi ya kujadili jambo hili kupitia vyombo vya maamuzi ikiwemo bunge ambalo lina mamlaka ya kubadili sheria huku akisisitiza kuwa hayo yakisubiliwa sheria ziendelee kufuatwa.

Akijibu swali kutoka kwa mwandishi wa habari juu ya baadhi ya ving’amuzi vilivyopewa leseni ya kuonyesha channel hizo bila malipo kutofanya hivyo mkurugenzi mkuu TCRA Mhandisi James Kilaba amesema analitambua na tayari limefanyiwa kazi.

Mwaka 2012 Tanzania ilizima rasmi mitambo ya analojia na kuingia kwenye mfumo wa digitali ambapo ving’amuzi vinne vilishinda zabuni ya kuonyesha channel tano za kitaifa bure ambavyo ndivyo vinaruhusiwa kufanya hivyo pekee na kilichotokea sasa ni ving’amuzi visivyokuwa na leseni hiyo kuonyesha pia channel hizo.