Katibu Mkuu CCM kutinga Zanzibar kwa mara ya kwanza


Na. Thabit Madai, Zanzibar
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk.Bashiru Ally anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku nne visiwani humu Agosti 17 hadi 20 mwaka huu.

Dk.Bashiru anafanya ziara hiyo kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo Mei mwaka huu baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu Abdulrahman Omar Kinana kustaafu.

Akitoa taarifa ya ziara hiyo ya Katibu Mkuu huyo, Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu Taifa(NEC),Idara ya Itikadi na Uenezi CCM, Zanzibar Catherine Peter Nao, alisema CCM Zanzibar tayari kimekamilisha maandalizi yote ya mapokezi ya kiongozi huyo.

Catherine alisema katika ziara yake hiyo pamoja na mambo mengine anatarajia kuzungumza na viongozi mbalimbali wa CCM na jumuiya zake na makundi ya kutoka taasisi za vijana visiwani humu.

Aliongeza kuwa ziara hiyo ya Dk.Bashiru itakuwa ni ya kikazi na kujitambulisha kwa wana-CCM ambapo wanatakiwa kujitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Katibu Mkuu huyo ambapo atawahutubia wanachama pamoja na wananchi kwa ujumla katika uwanja wa Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui saa 9 alasiri.

“Tunawaomba wanachama wote tujitokeze kwa wingi kushiriki mapokezi hayo ya kiongozi wetu mpendwa ambaye ni mara ya kwanza kuja tukitambulisha na kuzungumzia sera na masuala mbalimbali ya kuimarisha CCM na Jumuiya zake, alisema  Catherine.

Akizungumzia ratiba ya ziara hiyo Katibu huyo wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar,Catherine alisema siku ya siku ya kesho Agosti 17 mwaka huu katibu Mkuu huyo atakutana na kuzungumza na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Katibu huyo aliongeza kuwa Dk.Bashiru anatarajia kukutana na  na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.

Alisema mchana wa siku hiyo ya ijumaa atazuru Kaburi la Muasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Hayati Mzee Abeid Karume na kuzungumza na watumishi pamoja na Wazee wa CCM Zanzibar ambapo jioni atazungumza na Viongozi na wanachama wa Mikoa minne ya CCM Unguja hapo katika viwanja vya CCM Kisiwandui.

Catherine aliendelea kueleza kuwa jumamosi ya Agosti 18 mwaka huu Katibu Mkuu huyo atazungumza na Wenyeviti wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Makatibu wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Kamati za siasa za Mikoa na Wilaya, Wabunge, Wawakilishi na madiwani katika ukumbi wa Kamati Maalum Kisiwandui pamoja na kuzungumza na makundi ya vijana katika ukumbi wa CCM Mkoa wa mjini.

Aliongeza kuwa siku ya Jumapili Agosti 19, mwaka huu Katibu Mkuu huyo asubuhi atasafiri kuelekea Pemba kwalengo la kuendelea na ziara yake hiyo ambapo atazungumza na Watumishi wa CCM na  wazee  wa Pemba katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Kitengo.

Katibu huyo alisema Dk.Bashiru anatarajia kuzungumza na viongozi na wanachama wa CCM wa Mikoa miwili katika ukumbi wa skuli ya Fidel Castro Mkoa wa Kusini Pemba na jioni anatazungumza na Wenyeviti wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Makatibu wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Kamati za siasa za Mikoa na Wilaya, Wabunge, Wawakilishi,madiwani na maafisa wadhamini katika ukumbi wa Makonyo Pemba.

Katibu Mkuu huyo atahitimisha ziara yake hiyo siku ya Juma tatu Agosti 20 mwaka huu, kwa kuzuru kaburi la Dk.Omar Ali Juma kisiwani Pemba na kumalizia ziara yake kwa kuzungumza na  makundi ya vijana ambapo jioni atasafiri kuelekea Dar es salaam kuendelea na majukumu mengine.