8/10/2018

Mbunge wa CHADEMA Pascal Haonga aachiwa huru

Mahakama ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe imewaachia huru mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga na wenzake wawili baada ya kukutwa hawana hatia kwenye kesi iliyokuwa ikiwakabili.

Haonga, Wilfredy Mwalusamba (Katibu wake) na Mashaka Mwampashi walishtakiwa kwa makosa matatu yakiwemo ya kufanya fujo na kuvuruga mkutano wa uchaguzi wa baraz la mji mdogo wa Mlowo na kuwazuia askari katika kutekeleza wajibu wao.

Washtakiwa hao wameachiwa huru baada ya Jamhuri kushindwa kuthibitisha makosa dhidi yao.

Akisoma hukumu hiyo, hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Nemes Chami amesema katika mashtaka yote matatu, upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha makosa.

 Mbunge huyo na wenzake walidaiwa kutenda kosa hilo, Agosti 28, 2017 .

Tukio la kusomwa hukumu hiyo lilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji, mwenyekiti wa chama hicho kanda ya Nyasa, mbunge wa Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa na katibu wake, Emmanuel Mwasonga.