Samatta aungana na wanahabari kulaani Polisi kumpiga mwandishi


WAKATI Watanzania mbalimbali wakitoa matamko ya kulaani kitendo cha Mwandishi wa habari wa Wapo Redio Silas Mbise kushambuliwa na Polisi katika mechi kati ya Simba na Asante Kotoko Siku ya Simba Day mchezaji wa kimataifa na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’Mbwana Samata amesema kitendo hicho si cha kiungwana.

Samata ametoa kauli hiyo kutokana na kusambaa kwa video inayoonesha namna ambavyo mwandishi huyo akishambuliwa licha ya kujisamilisha.

Hivyo kutokana na video hiyo Samata kupita ukurasa wake wa Twitter ameelezea kusikitishwa na shambulio hilo.

Samata amesema hivi “Sio kitendo cha kiungwana askari kupiga mwandishi katika eneo la michezo , mpira ni mchezo unaoleta amani sio kuvunja amani.”.Wakati Samata akitoa kauli hiyo tayari leo mchana Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linalaani vikali tukio hilo linalosambaa mtandaoni la kupigwa kwa mwandishi huyo.

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amewaambia waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam amesema tukio hilo limetokea Agosti 8 mwaka huu siku ya mechi kati ya Simba na Asante Kotoko ya nchini Ghana.Aidha amesema Polisi Kanda Maalum imeanza uchunguzi wa tukio hilo kwa kufungua jalada la uchunguzi wa picha ya video hiyo inayosambaa na kuonesha askari polisi na mwandishi huyo wa habari ili kubaini ukweli.

Mambosasa amesema hiyo inakwenda sambasamba na kumtaka mtendewa wa kosa hilo la kupigwa kutoa taarifa kituo cha Polisi ili hatua stahiki zichukuliwe na kwamba mtu yoyote anatakiwa kutoa malalamiko yake pale anapoona ametendewa vitendo ambavyo ni kinyume na sheria.