Saudi Arabia yaahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania


Balozi Dkt.Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mohamed Ben Mansour Al Malek. Mazungumzo baina ya Viongozi wa Wizara na Balozi Mohamed yalijikita katika kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia baina ya Mataifa haya mawili (Tanzania na Saudi Arabia).

Aidha viongozi hao wamekubaliana kukamilisha maandalizi ya kongamano la biashara litakalo husisha wafanyabiashara na wadau wengine kutoka Saudi Arabia na Tanzania. Balozi Mohamed amebainisha kuwa ujumbe kutoka Saudi Arabia utakuwa na wafanyabiashara zaidi ya 40 wakiongozwa na Waziri wa Biashara wa Saudi Arabia.

Balozi Mohamed ameonesha nia yakuanzisha majadiliano kati ya Tanzania na Saudi Arabia ya kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Tanzania kwenda Saudi Arabia kwa lengo la kukuza biashara baina ya nchi hizi mbili.