8/10/2018

Serengeti Boys kupeperusha bendera ya Taifa kesho


Watanzania wangetamani kuona timu yao ya vijana inakwenda kucheza katika michuano mikubwa.

Safari itaanza kwa timu hiyo ya taifa ya vijana ya Tanzania ya U17, Sereneti Boys kucheza na Burundi katika michuano ya kuwania kufuzu kikanda Afrika Mashariki na Kati kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kesho.

Michuano hiyo inasimamiwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki (Cecafa) na Tanzania ipo kundi, A na timu za Rwanda, Burundi  na  Sudan, ikiwa ni baada ya Somalia kujitoa.

Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye Hotel ya Peacock jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye, amesema; "Tulikua na jumla ya timu 10, lakini timu moja imejitoa ambayo ni Somalia kwa sababu zisizojulikana, hivyo kundi A litabakiwa na timu nne, na kundi B litabaki na timu tano vilevile, na viwanja vitakavyotumika ni viwili tu ambavyo ni Uwanja wa Taifa, pamoja na Azam Complex.

Aidha, katika hatua nyingine Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo alisema kuwa “Michuano hii haitakuwa na kiingilio na lengo kubwa ni kutoa nafasi kwa wadau wa soka kujitokeza kwa wingi, inatoa fursa kwa 'Serengeti Boys' kujipanga na kujiandaa kama mwenyeji wa michuano ya AFCON mwakani."