Serikali yafanikiwa kuwadhibiti majangili wa Tembo


Serikali wilayani Tunduru mkoani Ruvuma imedhibiti matukio ya wananchi kuua Tembo na kula nyama yake  katika  vijiji vya Wenje na Mkapunda mpakani mwa  Tanzania  na Msumbiji kutokana na doria za mara kwa mara ambazo imekuwa ikizifanya kudhibiti vitendo vya ujangili.

Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Tunduru Bw. Juma Homera wakati akizungumza  na wananchi wa vijiji hivyo baada ya kukagua  mpaka wa Tanzania na Msumbiji  wa mto Ruvuma  kwa upande wa Tunduru akiongozana na mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Ruvuma Mndeme anazungumzia umuhimu wa wananchi kutunza amani iliyopo kwa kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali wanapowaona watu wanaowatilia shaka kwa kuwa wanaishi mpakani.

Kwa upande wao wananchi waishio  vijiji  vya Wenje na  Mkapunda  katika   kata ya Nalasi   wanaishukuru serikali kwa  azma  yake  ya kutatua baadhi ya kero zinazowakabili.

Miaka kadhaa iliyopita vijiji  vya Wenje na Mkapunda viliandamwa na matukio ya wananchi kuua Tembo na kula nyama yake huku wengine wakiondoka na meno yake lakini jitihada za serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali matukio hayo yamedhibitiwa.