Staa wa Singida United aelekea 'Sauzi' kwa majaribio


Klabu ya soka ya Singida United imethibitisha kuwa mshambuliaji wake Habibu Kyombo amepata nafasi ya kufanya majaribio kwenye klabu ya Mamelodi Sundowns baada ya timu hiyo kumuhitaji.

Mkurugenzi wa timu hiyo Festo Sanga amesema Mamelodi Sundowns ndio wamemuomba nyota huyo baada ya kumfuatilia kwa siku kadhaa na kuridhishwa na kiwango chake.

''Habibu yupo nchini Afrika Kusini tayari, anaanza majaribio ya siku 10 kwenye klabu ya Mamelodi Sundowns na sisi kama klabu tumebariki safari yake na tunamtakia kila la kheri'', amesema.

Kyombo amejiunga na Singida United kwenye dirisha la usajili la kiangazi mwaka huu, akitokea klabu ya Mbao FC ambako alifanya vizuri na kuwa mfungaji bora wa kombe la shirikisho nchini msimu uliopita.