Tanzania yashindwa kusogea, yazidiwa na Uganda FIFA


Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeeendelea kuganda palepale katika viwango vya soka duniani kwa mujibu wa listi ya shirikisho la soka duniani FIFA iliyotelewa leo, Agosti 16.

Taifa Stars imeendelea kushikilia nafasi ya 140 ikiwa nafasi nne nyuma ya Rwanda inayokamata nafasi ya 136 na nafasi nane juu ya Burundi ambayo inashikilia nafasi ya 148 katika viwango hivyo.

Uganda ‘The Cranes’ imeendelea kuongoza soka la Afrika Mashariki, ikisalia nafasi ileile ya 82 ya mwezi uliopita ikifuatiwa na Kenya iliyo katika nafasi ya 112 huku nafasi ya mwisho kwa nchi za Afrika Mashariki ikishikiliwa na Sudan Kusini ambayo ipo nafasi ya 156.

Kwa bara la Afrika, Tunisia inaongoza ikiwa katika nafasi ya 24 baada ya kuporomoka nafasi tatu nyuma toka mwezi uliopita, ikifuatiwa na Senegal iliyopo nafsi hiyohiyo ya 24 baada ya kupanda nafasi tatu tofauti ikiwa ni katika alama ambapo Tunisia ina alama 910 huku Senegal ikiwa na alama 838.

Bingwa wa kombe la dunia mwaka huu, timu ya taifa ya Ufaransa inaongoza katika nafasi ya kwanza ikiwa imepamda nafasi sita zaidi, ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2002 ikifuatiwa na Ubelgiji katika nafasi ya pili na Brazil inayokamata nafasi ya tatu.

Nafasi ya nne mpaka ya kumi ikishikiliwa na Croatia, Uruguay, Uingereza, Ureno, Uswisi, Hispania na Denmark kwa kufuata mpangilio wake.