Vikao vya majadiliano na wadau kuhusu ujuzi na stadi adimu za kazi vyaanza Dar


Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu (Idara ya Ajira kwa kushirikiana na Idara ya Kazi) wamefanya vikao vya majadiliano na wadau kuhusu ujuzi na stadi adimu za kazi katika soko la ajira kwa sekta ambazo ni chachu ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya rasilimali watu zikiwemo za Mafuta na Gesi, Afya, Viwanda, Elimu, Kilimo, Nishati, Ukarimu na Utalii, Ujenzi, Fedha na Bima, TEHAMA na Usafirishaji.

Akizungumza wakati wa kikao hiko Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo na Maendeleo ya Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Venerose Mtenga alisema kuwa vikao hivi na wadau kutoka kwenye sekta mbalimbali zilizopo nchini zitaleta mafanikio katika uandaaji wa orodha ya ujuzi na kada adimu za kazi katika soko la ajira.

“Tumeweza kupata maoni ya wadau juu ya kutokuwepo kwa sasa au hapo baadae kwa watu wenye vigezo au ujuzi fulani kulingana na mahitaji ya soko la ajira, hivyo mkutano huu umeweza kuwezesha kupata orodha ya ujuzi na kada adimu hapa nchini kutoka kwa wadau wa sekta hizo husika” alisema Mtenga.

Aliongeza pia orodha hiyo imekuwa ikiandaliwa kwa lengo kuu la kulinda ajira za wazawa, vilevile kuwasaidia wazawa kupata ujuzi na taaluma adimu kwa wageni ambao watakuja kufanya kazi nchini na kuongeza wigo wa taaluma ambazo hazipo nchini.

Naye Kamishna Msaidizi wa Kazi Bi. Mercy Jilala alisema kuwa kukutana na wadau hao kutasaidia kuandaliwa kwa orodha ya aina ya ajira au kazi zenye ujuzi adimu wanazoweza kufanya wageni ili kuweza kutoa vibali vya kazi nchini kwa kuzingatia vigezo na aina ya kazi zitakazo ainishwa.

“Ni vyema kila sekta ikatoa mapendekezo juu ya ujuzi au stadi adimu za kazi wanazoziona zinauhitaji mkubwa ili kusaidia upangaji na uendelezaji rasilimali watu, uwekaji sifa za kazi, uendelezaji wa mitaala, mikakati ya ajira na ” alisema Jilala

Kwa upande wake Dkt. Yusuf Kaderbhai kutoka Kituo cha Afya cha London (LHC) kilichopo jijini Dar es Salaam ameeleza kuwa majadiliano hayo yataleta mafanikio makubwa katika upatikanaji wa wataalamu kwenye baadhi ya sekta kutokana na ukosefu wa wafanyakazi wenye ujuzi au taaluma inayotakiwa na hivyo kusababisha ukosefu wa baadhi ya huduma.