Wafariki katika shambulio la wanamgambo

Watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wenye itikadi kali za dini ya kiislamu wamekivamia kijiji kaskazini mashariki mwa Nigeria, na kuwaua watu kadhaa.

Kuna taarifa za kutofautiana kuhusu idadi ya vifo vya watu huko Mailari, katika jimbo la Borno. Kiongozi mmoja wa sungu sungu katika eneo hilo ametaja kuwa ni watu 6 waliouawa lakini jamaa mmoja aliyeponea shambulio hilo ametaja kuwa ni watu 19 waliouawa.

Wanamgambo hao walikivamia kjiji hicho na kuwapora wakaazi kwa saa mbili kabla ya kuondoka, shahidi mmoja alisema.

Kundi la wanamgambo wenye itikadi kali za kiislamu Boko Haram limetekeleza mashambulio kadhaa katika jimbo hilo la Borno.

Kiongozi wa Sungusungu Babakura Kolo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa wanamgambo hao waliwasili katika magari makubwa Jumamosi usiku wakifyetua risasi na kurusha makombora.

"Katika purukushani hiyo, Boko Haram waliwakamata wanaume 6 na kuwakata shingo," Babakura Kolo amesema.

"Miili ya wahanga hao sita ilipatikana Jumapili asubuhi wakati wakaazi walipokuwa wanarudi katika kijiji hicho kilichoteketezwa."

Mkaazi Aisami Grema ameeleza kuwa polisi walio karibu hawakujaribu kukabiliana na washambuliaji.

Mkaazi mwingine, Abatcha Umar, amesema hana hakika iwapo washambuliaji hao walikuwa ni wafuasi wa kundi la Boko Haram au wa kundi lililojitenga la Islamic State katika jimbo hilo Magharibi mwa Afrika (Iswap).

Ameeleza kuwa wanamgambo wamekuwepo katika kijiji hicho siku tatu kabla ya shambulio hilo.

Boko Haram liliidhinisha uasi mnamo 2009 kwa lengo la kuidhinisha utawala wa kiislamu magharibi mwa Afrika.