wanawake wasioolewa hupangishwa nyumba kwa shida?

Wamiliki wengi wa nyumba za kupangisha nchini Nigeria wanawashuku wanawake ambao hawajaolewa kuwa wanajiuza miili yao na hivyo kuwapa wakati mgumu kupangisha nyumba zao.

Olufunmilola Ogungbile mwenye umri wa miaka 30 hakutegemea kwamba anaweza kulala sebuleni katika kiti cha rafiki yake kwa kipindi cha miezi mitano wakati anatafufa nyumba bila mafanikio katika mji wa Abeokuta huko kusini wa Nigeria licha ya kwamba ana kazi nzuri.

Olufunmilola alihama kutoka Lagos baada ya kupata kazi nzuri serikani ya kuwa meneja wa mradi .Pamoja na mafanikio ya kifedha ambayo dada huyo anayo lakini alikutana na changamoto kubwa ya kupata nyumba ya kuishi katikati ya mji au maeneo yaliyo karibu na masoko kwa sababu alikuwa hajaolewa.

"Swali la kwanza ambalo wapangishaji nyumba huwa wanauliza ni kama nimeolewa na ninapowajibu kwamba bado basi watauliza tena kwa nini?"

Na maswali hayo mara zote Bi. Ogungbile anadai kuwa huwa yanamshangaza sana.

"Kwanini kuolewa au kutoolewa kiwe kigezo cha kwanza mimi kupata sehemu ya kuishi?"Bi. Ogungbile aeleza, Bi. Ogungbile anasema ubaguzi wa namna hiyo umeenea sana

Bi. Ogungbile aliiambia BBC kwamba asilimia 99 ya wamiliki wa nyumba hawakutaka kunipangisha kwa sababu sijaolewa.

"Madalali wengi pamoja na wamiliki wa nyumba walinitaka nimpeleke mchumba wangu wakamuone"Walisema kwamba katika nyumba zao hawataki wanaume wawe wanaingia na kutoka ,wao wanataka mtu awe na heshima zake

Bi. Ogungbile anaamini kwamba changamoto ambazo amezipitia zinatokana na mila na desturi,watu wengi wanaamini kuwa mtu akiolewa ndio ana adabu na heshima.

"Upande huu wa dunia kama haujaolewa basi wewe ni kahaba",aliongeza

Wakati Sylvia Oyinda yeye ni meneja masoko mjini Lagos anakubaliana na kuepo kwa ubaguzi huo ambao unawapa wakati mgumu wanawake kupangisha nyumba nchini Ngeria.

Bi Oyinda, mwenye umri wa miaka 31,yeye alikuwa amechumbiwa wakati anatafuta nyumba na wenye nyumba walikataa kumpangisha mpaka wamuone mchumba wake kwanza.

Kuna misemo mingi ambayo inawanyooshea vidole wanawake ambao hawajaolewa ya kudhaniwa kuwa kuna wanaume wazee ambao wanawalipia kodi ya nyumba ..kwa mfano nchini Tanzania wanawaita 'Sponsa','buzi' au 'danga'.

Oyinda anaamini kwamba wamiliki wengi wa nyumba wanadhani kwamba wasichana wengi wasioolewa wanatabia hiyo ya kujiuza.

"Wenye nyumba watatu ambao nilikutana nao walikataa kabisa kunionyesha nyumba za kuishi na kuniambia wala nisijisumbue"

Baada ya usumbufu mwingi Oyinda aliamua kuwa anaongozana na mchumba wake ambaye sasa wameoana na waliweza kupata nyumba nzuri ya kupangisha.

Kwa upande wao wamiliki wa nyumba wao wanadai kutowabagua wanawake wasioolewa lakini huwa wanaangalia maslahi yao pia.

Coleman Nwafor ambaye ni mliki wa nyumba ya kupangisha anadai kwamba wateja wao wengi ni wanaume kwa sababu wanaume ndio wenye fedha nying zaidi.

"Wamiliki wengi wa nyumba wanataka mteja ambaye hatasumbua kulipa au kuongeza muda wa mkataba wake wa kupangisha wakati wanawake wengi ambao hawajaolewa wanawategemea wapenzi wao kuwalipia hivyo huwezi kujua nini kitatokea baada ya mwaka mmoja kuisha".