Waziri Kalemani azindua mtandao wa usambazaji gesi asilia


Waziri wa nishati Medard Kalemani amezindua mradi wa mtandao wa usambazaji gesi asili majumbani mkoani Mtwara huku akiliagiza shirika la maendeleo ya Petrol nchini TPDC kukamilisha usambazaji huo awamu ya kwanza katika kipindi cha miezi mitatu.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo ambao ulihusu ukataji wa utepe na pia kuonyeshwa ramani ambapo mtandao huo wa usambazaji gesi utapita, Waziri Kalemani amesema serikali imejipanga kuhakikisha gesi asili inatumika majumbani  bila kubagua na pia kwenye magari ili kuepuka matumizi ya mafuta, na hivyo amewataka wawekezaji kujenga viwanda vya kutengeneza vifaa vinavyohusu mradi huo nchini badala ya kuendelea kuagiza toka nje ya nchi.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa amesema mradi huo umeletwa mkoani huko kwa wakati muafaka, kwani utasaidia kuinua uchumi wa wananchi, na kuondoka na historia ya wananchi kuharibu mazingira kwa kukata miti kwa ajili ya kuni na kuchomaji mkaa.

Mapema akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Mkurugenzi wa TPDC Mhandisi Kapuulya Musomba amesema kwa kuanzia nyumba 125 zitapitiwa na mradi huo utakaogharimu shilingi Bilioni 1.3.