Waziri wa Ujenzi aiagiza Tanroads kumchunguza mkandarasi wa kichina


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amemuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Njombe, kumchunguza mkandarasi wa Kampuni ya China Henan International Cooperation (CHICO), anayejenga barabara ya Njombe-Moronga, kama ana wataalamu wa kutosha.

Kamwelwe alitoa agizo hilo katika Wilaya ya Wanging’ombe baada ya kukagua hatua zilizofikiwa katika mradi huo na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wake, ambao mpaka sasa umefikiwa kwa asilimia 14.

Barabara hiyo ina urefu wa kilometa 53.9 na inajengwa kwa kiwango cha lami. Amesema hana uhakika na kampuni hiyo kama ni wenyewe Chico waliozoeleka katika uendeshaji wa miradi mingi nchini hasa ya barabara.

“Sijaridhishwa na kasi ya huu ujenzi, Meneja wa Tanroads hakikisha unafuatilia kwa makini mradi huu na kubaini sababu zilizopelekea kusuasua kwa mradi na kuondoa wataalamu ambao wataonekana wanaudhaifu na kukwamisha mradi huu,” amesema Kamwelwe.

Amesema hakuna sababu ya mkandarasi huyo kuchelewesha mradi huo kwani vifaa na mitambo yote ipo katika eneo la kazi na tayari serikali imeshamlipa fedha alizozidai kwa asilimia 95.

Amemweleza mkandarasi wa Kampuni ya Chico kuwa serikali haitamuongezea muda wa kuikamilisha barabara hiyo na wananchi wanaiongojea kwa hamu kubwa, kwani serikali imewaahidi wananchi hao ambao tangu Uhuru hawajawahi kuiona lami.

Kamwelwe pia amekagua ujenzi wa mradi wa barabara ya Moronga-Makete yenye urefu wa kilometa 53.5, inayojengwa na mkandarasi Kampuni ya China Railway Seventh Group na kuridhishwa na kasi yake.

 Akitoa taarifa Meneja wa Tanroads Mkoa wa Njombe, Yusuph Mazana, alimweleza waziri kuwa changamoto ya miradi hiyo kubwa ni kazi za ujenzi kuanza katika msimu wa mvua nyingi na hivyo kupunguza kasi ya ujenzi wake.

Mbunge wa Jimbo la Wanging’ombe, Gerson Lwenge, ameishukuru serikali kwa hatua ya ujenzi wa barabara ya Njombe-Moronga kwani ni muhimu katika usafirishaji wa mazao ya misitu na viazi.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Njombe- Makete yenye jumla ya urefu wa kilometa 107.4 unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 na unatarajiwa kukamilika