Baada ya kipigo kutoka kwa West Ham, Manchester United waweka rekodi hii


Baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa West Ham United, klabu ya Manchester United imeendelea kuweka rekodi mbovu kwenye ligi kuu ya England.

Kwa mara ya kwanza Man United imepata pointi chache zaidi kwenye mechi 7 za mwanzo baada ya kufanikiwa kukusanya alama 10 pekee. Hii ni mara ya kwanza tangu ilipofanya hivyo msimu wa 1989/90 ambapo ilipata pointi 7 kwenye mechi 7.

Kabla ya ya leo Manchester United ndio ilikuwa timu inayoongoza kwa kushinda mechi nyingi za Ligi Kuu ikitokea nyuma kwa mabao 2-0 kwenye kipindi cha kwanza. Ilikuwa imeshinda mechi 6 ikiwemo ya msimu ulipita ambao walitoka nyuma kwa 2-0 na kushinda 2-3 dhidi ya Man City.

Kwa upande wa mlinda mlango David de Gea ambaye msimu uliopita alikuwa mwiba kwa washambuliaji, sasa amesharuhusu nyavu zake kuguswa kwenye mechi 6 kati ya 7 za mwanzo msimu huu.

Wakati West Ham wakifurahia ushindi wao mchezaji Felipe Anderson yeye ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa pili wa Brazil kufunga bao kwenye EPL ndani ya klabu ya West Ham akitanguliwa na Ilan Araujo.

Kabla ya mchezo wa leo West Ham ilikuwa imeshinda mechi moja tu kati ya mechi 19 za Ligi Kuu dhidi ya Manchester United. Ilikuwa imetoa sare 5 na kufungwa mara 13 huku ikishinda 3-2 mwezi Mei 2016. Sasa imeshinda mara 2 baada ya leo kushinda 3-1.