Chadema kufufukia Liwale? Mgombea wake arudisha fomu


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia kikao maalum cha kamati kuu iliyoketi jumatatu, Septemba 10, 2018, jijini Dar es Salaam, kimemteua Juma Rashid Upinde kuwa Mgombea Ubunge wa Jimbo la Liwale, katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 13, mwaka huu.

Kamati kuu ya CHADEMA imefanya uteuzi huo kutokana na mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho ya mwaka 2006.

Taarifa iliyotolewa na Chadema inamtaja Upinde kama mmoja wa wanachama wake waandamizi wa Kanda ya Kusini (Lindi, Mtwara na Ruvuma) akiwa ameshiriki kukijenga na kukiimarisha chama hicho.

Mgombea huyo tayari ameshachukua fomu ya kugombea ubunge na kukamilisha kuijaza ambapo asubuhi ya leo ameirejesha kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Liwale kwa ajili ya uteuzi.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Wananchi CUF, Zuberi Kuchauka kujiuzulu na kujiunga na CCM ambapo amerudishwa na chama hicho kugombea tena.

Hii ni karata nyingine kwa Chadema katika kutafuta nafasi ya kuongeza idadi ya wabunge wao ndani ya Bunge baada ya wabunge wao watatu kujiuzulu ambao ni Julius Kalanga wa jimbo la Monduli, Dk Godwin Mollel na Mwita Waitara wa jimbo la Ukonga.