.

9/14/2018

Davido aamua kujiunga na jeshi Nigeria, asitisha ghafla ziara yake ya muziki nchini Marekani

Msanii maarufu nchini Nigeria, Davido ametangaza kusitisha ziara yake ya muziki nchini Marekani aliyooita ‘THE LOCKED UP’ na kueleza mashabiki wake kuwa ataungana na jeshi la kujenga taifa la nchi hiyo ili aingie kwenye mafunzo maalumu ya kitaifa ya National Youths Corps Services (NYCS).

Davido kupitia ukurasa wake wa Instagram amewaomba radhi wanaigeria wenzake na kisha kutoa tangazo la kusitisha ziara yake nchini Marekani ili kuungana na wanafunzi waliomaliza vyuo nchini humo kwenye mafunzo hayo maalumu ya kijeshi.

Mapema mwezi uliopita Davido alitangaza kuwa ataungana na Jeshi la Kujenga Taifa la nchi hiyo ili kushiriki kwa hiyari kwenye mafunzo yanayotolewa kila mwaka kwa wanafunzi wanaomaliza vyuo nchini humo.

Davido ataungana na wanafunzi waliomaliza vyuo vikuu na vya kati nchini humo, kwenye mafunzo hayo maalumu kwa miezi mitatu Davido atakuwa akifanya mazoezi ya ukakamavu, kulima, kujenga, kufyatua tofali na shughuli nyingine kama ambavyo hapa nyumbani jeshi la JKT wanavyofanya.