https://monetag.com/?ref_id=TTIb Hii ndio kauli ya Wasira kuhusu chuo cha kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere | Muungwana BLOG

Hii ndio kauli ya Wasira kuhusu chuo cha kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere


Mwenyekiti mpya wa bodi ya utawala ya chuo cha kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere Steven Wasira amekipa changamoto Chuo hicho kuhakikisha taaluma inayotolewa na chuo hicho inaakisi maudhui ya mwasisi wa Chuo hicho Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Wasira ambaye aliteuliwa hivi karibuni na Rais Dk. John Magufuli kuwa mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam, alikuwa akizungumza kwa mara ya kwanza na wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya Chuo hicho alipofanya ziara ya utambulisho.

Amesema pamoja na wajibu wa chuo hicho kufundisha taaluma mbalimbali, bado kina wajibu wa kuboresha mafunzo ya uongozi na utawala kwa ajili ya viongozi, watumishi wa umma na sekta binafsi namna ya kuzingatia maadili, jambo ambalo mwalimu Nyerere alilitilia mkazo wakati wote wa maisha yake.

Chuo cha Kumbukubu ya Mwalimu Nyerere kilianzishwa mwaka 1958 kwa ajili ya kutoa mafunzo ya uongozi na baadaye kukabidhiwa serikalini kwa ajili ya kufundisha taaluma mbalimbali kimejijengea historia ya kuwaandaa viongozi wa nchi zilizokuwa mstari wa mbele wakati wa harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika.