https://monetag.com/?ref_id=TTIb Jinsi ya Kuepuka Kisukali, matibabu na lishe | Muungwana BLOG

Jinsi ya Kuepuka Kisukali, matibabu na lishe


Mpaka sasa hakuna dawa ya kuondoa moja kwa moja kisukari japokuwa watu wenye kisukari aina ya 2, baada ya kurekebisha vyakula wanaweza kujiweka katika hali ambayo mwili unaweza kutumia insulin yake kidogo bila ya kula vidonge au sindano.

Kwa sasa, insulini haiwezi kumezwa kama dawa za kawaida, kwani protini hiyo humeng’enywa kabla haijafika kwenye damu. Dawa za kisukari zatia ndani zile ambazo huchochea kongosho kutokeza insulini zaidi, nyingine hudhibiti ongezeko la sukari katika damu na nyingine hudhibiti ongezeko la sukari katika damu na nyingine huwezesha chembe za mwili kupokea insulini. Kuna utafiti wa kupandikiza (transplant) ili kuongeza insulin mwilini kwa kutumia sehemu ya kongosho (pancresase) ya mtu mwingine lakini bado haujafanikiwa kuweza kutumika kama matibabu.

Watafiti nchini Japan wamegundua jinsi seli za mfumo wa fahamu zinavyoweza kutumika kama seli mbadala zinazofaa kupandikizwa kwenye seli kongosho ili kutibu kisukari. Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti huo uliofanywa na taasisi ya tafiti za Afya ya AIST ya Tsukuba ya nchini Japan, ambayo imechapishwa kwenye jarida la kitafiti la (Embo Molecular Medicine) inaonesha kuwa seli zinazovunwa kutoka katika mfumo wa fahamu zinaweza kupandikizwa katika tezi kongosho na hivyo kumaliza tatizo la ukosefu wa seli za beta ambazo huhitajika kwa ajili ya uzalishaji wa insulini.

 Lishe kwa mtu mwenye kisukari

Baadhi ya nyakati mtu anaweza kufikwa na maafa kama misiba au matatizo ya kifamilia, hivyo mtu hupendelea kujiliwaza kwa kula zaidi au kupoteza hamu ya kula kabisa. Hali hizi zina athiri ugonjwa wa kisukari hivyo mtu inambidi aendelee na kula kama ilivyopendekezwa ingawa mara nyingine inaweza kuwa vigumu. Ni bora kuendelea kula milo midogo midogo ya mara kwa mara hii inasaidia kupunguza uzito wa mtu vile vile na kuifanya insulini kufanya kazi kwa kasi au ubora zaidi. Inawezekana kuwa huna njaa nyakati za kula, lakini inafaa utambue kwamba ni vyema ukila vitu vidogo vidogo vikavu kama ngano nzima na ule pamoja na tunda moja. Ulaji huu utakufanya usiwe na njaa kali wakati wa milo mikuu na kwa hivyo utakula kidogo zaidi.

Matunda ni chakula bora, lakini mengi yao yana sukari nyingi kwa hiyo ni vizuri kula si zaidi ya mawili-matatu kwa siku ukihakikisha kupunguza ulaji wa zabibu, embe, ndizi mbivu, matunda makavu kama tende, zabibu kavu, zeituni kwa vile matunda haya yana sukari nyingi. Mboga mboga ni vyakula bora na haziongezi sukari katika damu. Mboga mboga hizo hujumuisha  mabilinganya, bamia, vitunguu, kabeji, karoti, nyanya, tango na kisamvu. Pia vyakula vyenye mizizi huteremsha sukari katika damu mfano njegere, kunde, mbaazi, maharagwe, njugu mawe, muhogo, ndizi mbichi, magimbi na viazi vikuu.

Epuka vyakula vya utamu-utamu kama vile halua, jelebi, laddu-laddu, peremende-pipi, asali, matunda ya kuchemsha, jamu, keki na kashata. Pia jizoeshe kula vyakula visivyo vitamu tamu. Inafaa mtu anywe vinywaji vilivyo punguzwa utamu au kutiwa utamu wa vidonge yaani vinywaji bila sukari. Hakikisha kwa kusoma vinavyounda kinywaji unachokunywa. Vidonge vya utamu haviathiri kiwango cha sukari katika damu kwa hivyo mtu anaweza kutumia vidonge hivi kwa kutayarishia vyakula badala ya kutumia sukari ya kawaida. Vidonge hivi viko vya aina tofauti kwa mfano saccharin (sakkarin), cyclamate, acesulframe na aspartame (nutra-sweet).

Punguza kunywa maziwa kwani yana (lactose) kwa hivyo mtu anahitajiwa asinywe zaidi ya nusu lita kwa siku, hii ina maana maziwa aina mbalimbali kama mtindi na yoghurt bila ya matunda. Ukila jibini hakikisha shahamu iwe ya kiasi cha asilimia 18 ambayo ni sawa na gramu 18 kwa kila gramu 100 za jibini. Samaki ni wenye manufaa makuu kisiha na aina zote zinaruhusiwa. Usile mayai zaidi ya 2-3 kwa wiki.

Iwapo mtu atapatwa na magonjwa mengine juu ya ugonjwa wake wa kisukari, anatakiwa aendelee na matibabu yake ya kisukari kama kawaida. Na anategemewa apime sukari katika damu mara kwa mara zaidi kuliko kawaida kwa vile magonjwa mengine yanaweza kuifanya sukari ikapanda zaidi ingawa matibabu yanaendelea kwa ukawaida.

Wataalamu wa tiba hupendekeza kwamba watu wanaougua kisukari wabebe kitambulisho na kuvaa mkufu unaoweza kuwatambulisha. Kitambulisho hicho kinaweza kuokoa uhai hali ya dharura ikitokea kwa mfano mtu aliyepungukiwa sukari mwilini anaweza kueleweka kimakosa kuwa ana ugonjwa mwingine au kwamba yeye ni mlevi. Pia mtu anapokuwa safarini anashauriwa kukumbuka kuchukua dawa zake na kupima sukari yake pale inapobidi.

Mtu anaweza kujiuliza itakuaje nikipata mialiko ya sherehe zenye vyakula vingi ambavyo havipendekezwi kwa wagonjwa wa Kisukari? Ikiwa mtu anafuata mapendekezo ya hapo juu, anaweza mara moja au mbili kwa mwezi kula mapocho pocho kama vile kwenye shughuli, mialiko, sherehe yenye vyakula vyenye mafuta, siagi na sukari kwa wingi.

 Athari zake

Watu wanaougua kisukari hawafi moja kwa moja kutokana na ugonjwa huo, bali hufa kutokana na magonjwa mengine kama ifuatavyo:-

Matatizo ya moyo; magonjwa ya moyo huwa mara mbili zaidi ya watu walio na kisukari, shinikizo la damu la juu kupita kiasi na kiharusi/kupooza(stroke), kuharibika mishipa ya damu na mishipa ya fahamu (Nerve Damage/Diabetes Neuropathy) hali hii husababisha ganzi inayopunguza hisia kwenye miguu na kupelekea kutohisi maumivu haswa miguuni (Diabetic foot) mfano unaweza vaa viatu vya kubana lakini usihisi hivo hata kupelekea vidonda na hata gangrini ya miguu. Kisukari ni sababu moja kubwa ya watu kukatwa miguu.

Kuharibika figo(Diabetes Nephropathy): Duniani kote kisukari ndio sababu kubwa ya figo kushindwa kufanya kazi(Kidney Failure), kuharibika macho (Eye damage/Diabetes Retinopathy): Sukari inaharibu mishipa ya damu iliyopo kwenye macho na kupelekea matatizo kwenye kuona na ukipofu. Duniani kote kisukari ndio sababu kubwa ya upofu kwa watu wazima. Kupungua nguvu za kupambana na maambukizo (kudhorota kwa kinga ya mwili), maambukizo ya fizi, ngozi, njia ya mkojo na ukeni na kifua kikuu huwa zaidi ya mara mbili kuliko watu wasio na kisukari.

Kupungua nguvu za kufanya kazi, kupungua nguvu za kiume(Electile Dysfunction) na hivyo kuharibu uhusiano ndani ya ndoa, inasababishwa na kutokuwa na msukumo wa damu wa kutosha kwenye uume kwa sababu mishipa ya damu hupungua upana/ukubwa kutokana na kugandana kwa sukari(Calcification). Karibu robo ya wanaume wote huwa na tatizo hili wakishindwa kudhibiti kisukari. Kuathiri uchumi kutokana na matibabu ya muda mrefu, tiba ya kisukari ni ya maisha. Mahitaji ya dawa peke yake hayapungui Sh 400,000 kwa mwaka kwa mgonjwa anayehitaji insulini.

 Jinsi ya kuepuka kupatwa na kisukari

Kuna aina kuu mbili za kisukari. Aina ya kwanza huanza hasa utotoni na kufikia sasa madaktari hawajui jinsi ya kuizuia. Ingawa zamani aina ya pili ilihusianishwa tu na watu wazima, hivi karibuni imewaathiri pia watoto. Sehemu hii inazungumzia aina ya pili ambayo imeathiri asilimia 90 ya watu walio na kisukari.

Kufanya yafuatayo kunaweza kukuepusha na kupatwa na Kisukari :-

Pima kiwango cha sukari kwenye damu ikiwa una uwezekano mkubwa wa kupata kisukari, jitahidi kula vyakula vyenye lishe, punguza kiasi cha chakula unachokula, badala ya kunywa vinywaji vyenye sukari nyingi au vinywaji vyenye kaboni kama vile soda, kunywa maji, chai au kahawa, kula vyakula vya nafaka ambayo haijakobolewa badala ya vyakula vilivyochujwa sana viwandani na kula nyama isiyo na mafuta mengi, samaki, njugu, karanga na maharagwe.

Fanya mazoezi. Kufanya mazoezi kunaweza kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu na kukusaidia uwe na uzito unaofaa. Kwa kupata lishe bora na kufanya mazoezi ya kutosha watu wengine wanaougua ugonjwa wa kisukari wa Aina ya pili wameacha kutumia Insulin angalau kwa muda fulani.

Uchunguzi mkubwa uliofanywa kwa wanawake ulionyesha kwamba kufanya mazoezi kidogo tu huongeza uwezo wa chembe za mwili wa kufyonza glukosi kwa msaada wa Insulin kwa zaidi ya saa 24. Hivyo, ripoti hiyo inakata kauli hii: Kutembea na kufanya mazoezi mengi hupunguza uwezekano wa wanawake kupata ugonjwa wa kisukari wa aina ya pili. Wachunguzi hao wamependekeza watu wafanye mazoezi ya kiasi kwa angalau dakika 30 na ikiwezekana kila siku.

Mambo mengine ni pamoja na kupunguza unywaji wa pombe wa kupita kiasi, kutotumia sigara au aina yoyote ya tumbaku, kujikinga na mfadhaiko kwa kuepuka msongo wa mawazo kwa maana mfadhaiko huongeza sana kiwango cha sukari katika damu.

Ikiwa unayo historia katika familia, si lazima kwamba utapata ugonjwa huu. Lakini kwa wale ambao wanaweza kuupata wanaweza kuuchelewesha kwa kujitahidi kuishi maisha ya afya nzuri kwa kula vyakula bora hasa mboga mboga kwa wingi, mazoezi na kujiepusha na uzito mkubwa wa mwili. Pia kupima damu baada ya kila mwaka ikiwa una historia katika ukoo au una wasiwasi kutokana na dalili za kisukari.