Jinsi ya kufanya uwekezaji wa biashara ndogo na kati


Hassani Mnyone mnyonehans@gmail.com
Biashara imara huanzishwa kwa ufanya upembuzi yakinifu ambao hutoa fursa kutambua mambo mengi kuhusu biashara yenyewe na mazingira ambayo biashara hiyo itawekezwa.

Biashara kubwa za kampuni hutumia fedha nyingi kufanya maandalizi ya msingi kabla ya kujiridhisha kama biashara hiyo inaweza kufanyika na kuleta matokeo chanya kwa wamiliki na wadau wengine.

Hili linaweza kufanyika kwa biashara aina zote na kiwango chochote cha mtaji ili kuziweka biashara katika maeneo salama. Uwekezaji wa biashara zote ni muhimu kuangalia mambo yafuatayo,

Upatikanaji wa malighafi au bidhaa za msingi za Biashara husika, ni muhimu sana kufungua na kuanzisha biashara eneo ambalo kutakuwa na urahisi wa upatikanaji malighafi muhimu kwa uzalishaji wa bidhaa kuu na huduma zinazotolewa na biashara husika.

Ili uimudu biashara ni lazima kujihakikishia upatikanaji wa malighafi au mizigo unayochukua kuleta kuuza iwe ndani au nje ya nchi ni muhimu kuwa na uhakika wa upatikanaji wa huduma na bidhaa zako.

Kuwafahamu wapinzani wako kwenye biashara unayokwenda kuwekeza, ili kuweza kuipata nafasi yako kwenye soko la ushindani. Wafahamu watu wanaofanya biashara kama yako au nyingine zinazofanana na yako.

Unawahitaji hawa ili kujua mapungufu yao na nguvu zao zilipo ili uone ni mbinu gani zitakusogeza mbele yao na ufanye vizuri zaidi ya wanavyofanya wao. Mikakati yako ya kimasoko na bei itakuwa mizuri ukianzia pale wenzako walipoishia. Kampuni za simu Tanzania zimekuwa mfano mzuri kwenye hili.

Kulifahamu soko la bidhaa na mahitaji ya wateja na wadau wako, ubunifu wa bidhaa zinazokwenda na wakati ni jambo la muhimu sana kwasababu sio kila bidhaa yako inafaa kutumika kwa watu wote.

Ni muhimu kulifahamu soko lako na ulichambue vizuri ili uweze kubuni bidhaa na huduma zinazokwenda na mahitaji yao. Mfano wa kampuni ya simu kwa ubunifu wao mzuri wa vifurushi vingi kama vile vya chuo ambako huko kuna wanafunzi wengi na wanatumia sana simu na vifaa vingine kufanya mawasiliano ya mtandao na kawaida, huu ni mfano wa biashara inayotambua soko lake na mahitaji ya wadau kutokana na mazingira.

Gharama za kuendesha Biashara yako, kuna wakati unaweza kuwa na wazo zuri sana la biashara lakini katika kufanya Uchunguzi na upembuzi ukagundua kuwa gharama za uendeshaji wa biashara yako zitakuwa juu na kukufanya upate hasara au kuendesha biashara isiyokuwa na tabia ya kupanuka ni vizuri kufikiria mara mbili kuhusu biashara hiyo.

Gharama za kuendesha biashara ni zile zinazohusisha malipo ya wafanyakazi, usafirishaji wa bidhaa, pango la eneo la kufanyia biashara na nyingine. Kama biashara inakupekeleka kwenye gharama kubwa zaidi ya faida basi ni vyema ukalipitia upya wazo lako ili kuwekeza sehemu salama yenye tija.

Utaratibu wa ulipaji kodi na gharama nyingine, ni muhimu na lazima kulipa kodi kwa biashara yoyote ila kama biashara yako unaona inaingia kukupa gharama kubwa na mazingira yasiyokuwa rafiki kwenye ulipaji kodi ni vizuri kujitathimini na kuangalia upya mfumo wa kuingiza au kuendesha biashara yako.

Hali ya eneo lako la biashara. Moja kati ya vitu vya muhimu sana kwenye biashara inayoanza au ile inayoendelea ni kujiuliza kuhusu eneo ambalo biashara yako unahitajika kuiweka.

Biashara nzuri inategemea eneo ambalo ofisi na majengo yake yatakuwepo kama yatakuwa katika maeneo sahihi kwa watu na wadau wake kufika na kupata huduma basi biashara hii itakuwa inafanya kazi nzuri lakini ukichagua eneo baya na ambalo haliendani na aina ya biashara yako unaweza kujikuta unapunguza nguvu ya biashara yako kufanya vizuri.