Mahakama yaamuru wafuasi Chadema kukamatwa


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar Es Salaam, imetoa hati ya kukamatwa kwa washtakiwa saba kati ya 31 wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo  (Chadema),
wanaokabiliwa na tuhuma za kufanya mkusanyiko isivyo halali.

Amri hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Augustino Rwizire, jana wakati kesi hiyo ilipopangwa kutajwa na washtakiwa hao kushindwa kufika Mahakamani.

"Kwa kuwa washtakiwa wameshindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi inapopangwa, Mahakama inatoa hati ya kukamatwa," alisema Hakimu Rwizire.

Washtakiwa waliotolewa na hati ya kukamatwa ni Edna Kimoro, Ramadhan Mombo, Ezekiel Nyenyembe, Raphael Mwaipopo, Athuman Mkawa na Jackson Masilingi.

Awali, Wakili wa Serikali Faraji Nguka, alidai mahakamani kuwa kesi hiyo imepangwa kwa ajili ya kutajwa lakini kuna baadhi ya washtakiwa katika kesi hiyo, hawajafika mahakamani hapo bila taarifa.

"Kutokana na washtakiwa hawa saba kutohudhuria kesi yao kwa muda mrefu, naiomba mahakama itoe hati ya kuwakamata washtakiwa hawa," alidai Nguka.

Baada ya kueleza hayo, hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 11, mwaka huu, itakapotajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Mbali na washtakiwa hao saba, wengine katika kesi hiyo ni Tabitha Mkude, Haji Lukwambe, Emmanuel Kimoi, Mohammed Juma, Hussein Mrombo, Abdallah Hamis, Hussein Kidda, Paulo Kimoro, Brayan Morris, Hussein Nguli na Edna Kimoro.

Wengine ni Jonathan Lema, Salha Ngondo, Ramadhan Mombo, Godwin Mwakasungura, Hassan Kibweda, Omary Hamad, Fatima Ramadhan, Ezekiel Nyenyembe, Denis Mtegwa, Dickson Kerefu, Raphael Mwaipopo, Athuman Mkawa, Mussa Kusigila.

Pia wamo Omary Danga, Jackson Masilingi, Asha Kileta, Ally Rajabu, Isack Ng'aga, Erick John na Aida Olomi.

Washtakiwa wanadaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu, huko Kinondoni katika eneo la Mkwajuni, Wilaya ya Kinondoni walifanya mkusanyiko usio wa halali na kinyume cha sheria.

Ilidaiwa kuwa mkusanyiko huo ulikuwa na nia ya kufanya uvunjifu wa amani na kusababisha taharuki kwa wananchi.