Rais Magufuli aungwa mkono vita dhidi ya rushwa na ufisadi


Na Ferdinand Shayo, Arusha
Taasisi wanachama wa Umoja wa Taasisi za Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki (EAAACA) zimekubaliana kuimarisha uchunguzi wa kesi za rushwa na ufisadi pamoja na kuhakikisha kuwa wahusika wanarejesha mali walizozipata kifisadi ili kutokomeza vitendo vya Rushwa.

Makamu wa Raisi wa Umoja huo Michael Mubea amewaambia wanahabari jijini Arusha kuwa licha ya watu wengi kushikiliwa kwa tuhuma za rushwa kumekua na changamoto ya ushahidi pamoja na urejeshwaji wa  mali zinazotokana na ubadhirifu wa mali za umma jambo ambalo wananchi wa Afrika Mashariki wanatazamia katika taasisi za kupambana na rushwa.

Aidha amesema kuwa kwa sasa wanaandaa mikakati ya kushirikiana kwa nchi zote wanachama iwapo kuna wahusika wa vitendo vya rushwa wanaoficha mali zao nchi jirani kuweza kugunduliwa na kuchukuliwa hatua stahiki.

“Tunampongeza Rais Magufuli katika mapamabano dhidi ya rushwa na ufisadi amekua mfano wa kuigwa jambo ambalo linawapa imani na matumani Watanzania na wananchi wa jumuiya ya Afrika Mashariki” Alisema

Raisi wa Umoja huo Wedo Atto amesema kuwa nchi za Afrika Mashariki zoitaendelea kushirikiana katika mapambani dhidi ya rushwa kwani rushwa ni kansa na ni tishio la maendeleo ya nchi yeyote.

Alisema kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanapaswa kuwa kipaumbele kwa nchi zote za Afrika Mashariki ili kuweze kupiga hatua kwa maendeleo ya Nchi.