Simiyu kunufaika kupitia mradi wa kitalu nyumba, Mavunde awaahidi neema


Na James Timber, Simiyu
Vijana takribani 4200 hapa nchini wanatarajia  kunuafaika na kilimo kupitia mradi wa kitalu nyumba (green house), ambao utaanza kutekelezwa katika mikoa sita ambayo imekuwa kinara kwa kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana, ukiwemo mkoa wa Simiyu na Halmashauri zake zote sita.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri , Ofisi ya Waziri Mkuu,  Sera, Bunge,  Kazi ,Vijana Ajira  na Walemavu Anthony Mavunde wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu yenye lengo la kukagua maeneo ya ujenzi wa vitalu nyumba na uwepo wa maji yatakayotumika katika  kilimo cha umwagiliaji.

Mvunde amesema katika kutekeleza mradi huo vijana watawezeshwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili iwe sehemu ya ajira yao, ambapo vijana watafundishwa kulima kwa tija kupitia kitalu nyumba na kujua namna ya kutengeneza vitalu nyumba na wananchi wengine wanapohitaji kujifunza namna ya kutengeneza vitalu nyumba wajifunze kwao.

“Tutaleta green house (Kitalu nyumba) ambayo itafungwa hapa na vijana wataelekezwa kulima kupitia huko, lakini pia tutawaunganisha na chama cha Wauza mboga Tanzania kwa ajili ya kutengeneza masoko ya uhakika ili green house (kitalu nyumba) hizo ziwe na tija” alisema Naibu Waziri Mavunde

Akiwa katika ziara yake Naibu Waziri huyo amekutana na baadhi ya vijana ambao watatekeleza mradi huo na kuwapongeza kwa uamuzi waliochukua na akatoa rai kwa vijana wote nchini kuacha kukaa vijiweni na badala yake wajishughulishe na teknolojia hiyo ili waondokane na umasikini.

Mkuu wa Mkoa wa Anthony Mtaka  ameishukuru Serikali kwa mpango huo ambao utawasaidia vijana kujiajiri kupitia vitalu nyumba na akamhakikishia Naibu Waziri kuwa mkoa wa Simiyu utahakikisha vijana wanafanya vizuri katika mradi huo

Hivi karibuni akiwa mkoani Simiyu Rais Dk John Magufuli alimtaja RC Mtaka kama Mkuu wa Mkoa bora katika Serikali yake.