.

9/14/2018

Simiyu yaahidi kutoa ardhi bure kwa wawekezaji

Na James Timber, Simiyu

Mkoa wa Simiyu umeandaa mazingira wezeshi kwa wawekezaji katika Fursa  mbalimbali za uwekezaji ambapo imejipanga kutoa ardhi bure kwa wawekezaji.

Mkuu wa Wilaya ya Wilaya ya Bariadi  Festo Kiswaga  amesema hayo alipokuwa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa Anthony Mtaka katika Ufunguzi wa Kongamano la Uwekezaji la Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali  Waadiventista Wasabato (ATAPE), lililofanyika Mjini Bariadi.

“Mkoa wa Simiyu una fursa nyingi mkifika hapa chagueni tu sehemu mje kuwekeza, mtu atakayekuja kujenga kiwanda kikubwa, kizuri ardhi tutampa bure, sisi tutamuuliza tu kwamba tuandike jina gani kwenye hati na tutamkabidhi hati yake, kwa hiyo ATAPE pelekeni salamu kwa wawekezaji wenzenu kuwa ardhi ya uwekezeaji Simiyu ni bure, ninyi mtafute mtaji tu,” alisema Kiswaga.

Ameongeza kuwa wawekezaji wote watakaowekeza mkoani Simiyu watapata soko la uhakika la bidhaa zao, huku akibainisha kuwa mkoa wa Simiyu na mikoa inayouzunguka ina wakazi wasiopungua milioni 10 ambao watakuwa wanunuzi wakubwa wa bidhaa zao watakazozalisha.

Aidha, Kiswaga ametoa wito kwa wawekezaji wote wakiwemo ambao ni wanachama wa  Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali  Waadiventista Wasabato (ATAPE), kuwekeza katika ujenzi wa hoteli na hosteli katika Eneo la Nyakabindi mahali ulipo Uwanja wa Nanenane Halmashauri ya Mji wa Bariadi ili kukabiliana na changamoto ya malazi.

Katika hatua nyingine Kiswaga ametoa wito kwa Taasisi za Madhehebu ya Dini kuiga mfano wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali  Waadiventista Wasabato (ATAPE) katika  kuwajenga waumini wao kiroho na kuwaimarisha kiuchumi, ili Taasisi kama hizo zitumike kama madaraja kuwavusha waumini wao kueleka katika Uchumi wa Kati.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali  Waadiventista Wasabato (ATAPE), Bw. Fredy Manento amesema pamoja na kutoa huduma za kiroho ATAPE inatoa mafunzo ya  ujasiriamali,  imeweza kuwafikia zaidi ya wananchi 20,000 kupitia huduma za afya za bure na imewekeza zaidi ya shilingi milioni 639 katika miradi mbalimbali.

Makamu Mwenyekiti wa ATAPE Taifa (Upande wa Uwekezaji) Dkt. Dastan Kabiaro amesema katika uwekezaji huo ATAPE imeanza na kilimo ambapo  imeshanunua jumla ya ekari 10,250 katika mikoa ya Tanga, Iringa, Pwani , Njombe na inatarajia kupata eneo jingine katika Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kilimo cha miwa ya sukari.

“ATAPE imeanza kuwekeza katika kilimo,baadaye tutaenda kwenye maeneo mengine ambayo tumeshaanza kama maji, tutatoa visima \Tanzania nzima kwenye  maeneo yote ambayo hayana maji; katika kilimo tumeanza kuchukua ardhi na kuiendeleza mpaka sasa tuna ekari 10,250, tumeendeleza ardhi hiyo kwa asilimia 10 na tunaendelea kuiendelea ardhi hiyo” alisema.

Mwenyekiti wa ATAPE Kanda ya Bariadi, Bi. Mariam Manyangu amesema  mkoa wa Simiyu una wanachama takribani 80, ambao miongoni mwao ni watalaam katika fani mbalimbali pamoja na wafanyabiashara na wanaendelea kuhamasisha waumini wengi kujiunga na chama hicho,  ili kujenga waumini imara kiuchumi watakaoweza  kuendesha maisha yao na kuchangia kazi ya Mungu.