Wanaume Moshi waongoza kwa kupima Ukimwi


Na Ferdinand Shayo,Killimanjaro

Wanaume wa Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wameonyesha mwamko mkubwa katika kampeni ya kimkoa ya upimaji  wa afya kwa hiari ukiwemo ugonjwa wa ukimwi tofauti na miaka ya nyuma baada ya kupata elimu ya kutosha juu ya ugonjwa huo na magonjwa mengine yasiyoambukiza.

Taarifa hiyo imetolewa na Mratibu wa UKIMWI mkoani Kilimanjaro Dr .Eligy Mosile katika uzinduzi wa kampeni hiyo ambayo itazishirikisha wilaya zote za mkoa huo  hadi novemba 30 mwaka huu katika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu.


Dr. Mosile amesema, kwa siku tatu za awali za kampeni hiyo iliyoanza septemba kumi wanaume 903  wamejitokeza kupima afya zao kati ya wananchi 1,369 miongoni mwao 11 wamegunduliwa kuwa na virusi vya ukimwi wakiwemo wanaume sita  na wanawake watano na kuanzishiwa dawa..

Akizindua kampeni hiyo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dr.Anna Mghwira amesema, kiwango cha maambukizi ya ukimwi kimepungua kutoka asilimia 7.3 hadi asilimia 2.6   na kuonyesha takwimu hizo zitaendelea kupungua mwaka hadi mwaka kutokana na elimu inayotolewa na mashirika mbalimbali.

Mkazi wa Moshi Bw Deogratias mwacha anayeishi na virusi vya ukimwi kwa ujasiri kwa miaka 15 ameiomba serikali iwajengee uwezo wa kwenda kutoa elimu juu ya ukimwi katika taasisi mbali mbali mkoani kilimanjaro likiwemo jeshi la polisi na magereza.